AKAMATWA KWA KUSAFIRISHA MANANASI KWENYE GARI LA WAGONJWA



Dereva wa kituo cha afya cha Kebisoni IV wilayani Rukungiri Nchini Uganda amekamatwa baada ya kukutwa akisafirisha mananasi kwenye gari la wagonjwa la kituo hicho.

Akithibitisha tukio hilo Msemaji wa polisi kanda ndogo ya Kigezi, Elly Maate alimtaja dereva huyo kuwa ni Matayo Barekye, mwenye umri wa miaka 50, mkazi wa selo ya Nyakabare, halmashauri ya mji wa Kebisoni wilayani Rukungiri Nchini Uganda.




Amesema kuwa Mnamo Januari 27, 2022 Barekye alimsafirisha mgonjwa wa kike ambaye alikuwa amefanyiwa upasuaji kutoka Rukungiri hadi nyumbani kwake wilayani Ntungumo ambapo wakati akiwa njiani kurudi, alipigwa picha akishusha mananasi kutoka kwenye gari la wagonjwa alilokuwa akiendesha.

"Polisi walimkamata mshukiwa baada ya picha za hizo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na atashtakiwa kwa makosa ya utumizi mbaya wa ofisi,” Bw Maate alisema.


Aidha Msemaji wa Polisi Maate ametoa wito kwa watumishi wa umma kuzingatia kanuni za maadili kila mara ili kuepuka vishawishi hivyo vinavyowapelekea kuwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Mwisho

Post a Comment

Previous Post Next Post