Imeelezwa kuwa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kimila na Viongozi wa Serikali wana wajibu wa kutoa elimu juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 2022 ili wananchi waweze kutoa ushirikiano pamoja na kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kufanikisha lengo la zoezi hilo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati akizindua Semina ya Sensa ya Watu na Makazi iliyotolewa kwa viongozi wa Dini na wa Kimila ambayo imeandaliwa na Taasisi ya Dini ya Kiislamu ya TWARIQA ambapo amesema Sensa hiyo itasaidia upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia utekelezaji wa Dira ya maendeleo ya taifa.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote waliopo ndani ya nchi kwa umri, jinsia,mahali wanapoishi, hali ya elimu, ajira, vizazi, vifo na makazi ambapo misingi hiyo ndiyo inayoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi yenye uhitaji maalum kama vile watu wenye ulemavu, watoto, wanawake, vijana na wazee.
“Natambua viongozi wa Dini zote na viongozi wa Kimila wana jukumu kubwa la kuwa viungo kati ya serikali na wananchi na ili kudumisha amani kupitia nyumba za ibada kwa kufundisha maadili mema kama vitabu vitakatifu vinavyoelekeza na Nina imani viongozi wote mliokuja Leo mnauwezi wa kuelimisha jamii kutokana na nyazifa zenu,” Amesema Dkt. Kiruswa.
Pia, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, umuhimu wa Sensa ni pamoja na serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, kuboresha huduma za kijamii na kutoa viashiria vya maendelo.
Dkt. Kiruswa amesema takwimu za Sensa ya Mwaka 2012 zilionesha kuwa idadi ya watu ni zaidi ya million 44, wanaume wakiwa ni zaidi ya milioni 21 sawa na asilimia 48.7 na wanawake zaidi ya milioni 23 sawa na asilimia 51.3, huku milioni 31 sawa na asilimia 70.1 wanaoishi vijijini na milioni 13 sawa na asilimia 29.6 wakiishi mijini.
Sambamba na hayo, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, katika Sensa itayofanyika Agosti Mwaka huu, Wizara ya Madini inatarajia kuweka dodoso litakalosaidia kukusanya taarifa za wachimbaji wa madini wakiwemo vijana na wanawake ili kuweza kujua mahitaji yao hivyo wachimbaji wote nchi nzima wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zao kwa usahihi.Kwa upande wake, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Arusha Leokadia Mtey amesema kuwa Sensa itaisaidia serikali kupanga mipango mbalimbali ya kimaendeleo kwani inategemea takwimu katika kufanya shughuli za maendeleo ya nchi ambapo sensa hiyo itakuwa ni sensa ya 6 tangu nchi kupata Uhuru mwaka 1961.
Athanas amesema kuwa, watu wanaostahili kuhesabiwa ni watu wote waliolala ndani ya mipaka ya Tanzania ambapo lengo kuu ni kuhakikisha kwamba kila mtu aliyelala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa anahesabiwa na atahesabiwa mara moja.
“Sensa inayoenda kufanyika ipo kiutaratibu na miongozo na taarifa zote binafsi za watu zitakazokusanywa ni siri na zitatumika kwa madhumuni ya takwimu tuu hivyo wananchi msiogope kutoa taarifa sahihi kwani wakitoa taarifa za uongo itafanya serikali ipange mipango ambayo haitakiwa na manufaa kwa wananchi,” amesema Mtey.
Naye Katibu wa Taasisi ya Twariqa Tanzania Yahaya Athman Mkindi amesema kuwa zoezi hili ni muhimu kwa kuwa litawasaidia serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta ya mbali mbali kama elimu,afya,hali ya ajira,miundombinu ya barabara nishati na maji safi.
Awali Dkt. Kiruswa alitembelea Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha ambapo alizungumza na watumishi wa ofisi hiyo na kuwataka waongeze juhudi na maarifa kwenye utendaji kazi wao ili lengo la Wizala la kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifia ifikapo 2025 liweze kufikiwa.
Pia, Dkt. Kiruswa ametembelea Kituo cha Gemolojia Tanzania (TGC) kwa lengo la kujitambulisha kwa watumishi baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kumteuwa na kumwapisha kuwa Naibu Waziri wa Madini pamoja na kujionea jinsi gani shughuli za uongezaji thamani madini zinafanyika katika kituo hicho.
Mwisho
Post a Comment