Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameagiza kusimamiwa kwa Maafisa Ugani ili kutenda kazi zao kwa ufanisi unaotakiwa.
Akizungumza leo tarehe 17 Januari 2022 wakati akifungua kikao kazi cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na wakuu wa idara za Mifugo na Uvuvi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa (Tamisemi) kilichofanyika Ukumbi wa Kambarage Jengo la Hazina mkoani Dodoma Dkt Mpango amesema serikali itaendelea kuipa umuhimu Sekta ya Mifugo hapa nchini kutokana na mchango mkubwa wa sekta hiyo katika kuwainua wananchi kutoka katika lindi la umaskini kwa kutoa ajira na fursa mbalimbali.
Ameagiza kila Afisa Ugani kuwa na orodha ya wafugaji anaowahudumia, ratiba ya kuwatembelea wafugaji ili kuwashauri na kufuatilia maendeleo ya mifugo, na kupima matokeo ya huduma anazotoa.
Amesema kuwa licha ya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa idadi ya mifugo Barani Afrika lakini bado tija ya sekta hiyo hairidhishi kutokana na kukosekana kwa huduma bora za ugani pamoja na wananchi kuendeleza utamaduni wa ufugaji wa kienyeji ambao hauzingatii ubora bali idadi kubwa ya mifugo, hali inayopelekea uwezo mdogo wa kukabiliana na magonjwa ya mifugo, upungufu wa malisho na uharibufu mkubwa wa mazingira na vyanzo vya maji.
Aidha kutokana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, Makamu wa Rais amewataka watendaji wa Serikali katika ngazi zote kutoa elimu na kusimamia ufugaji kwa utaratibu wa kuingiza mifugo katika maeneo yenye malisho ili kupunguza migogoro ya ardhi pamoja na uharibifu wa mazingira.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekabidhi pikipiki 300 kwa wakuu wa Mikoa wakiwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ili kutumika kwa kazi za maafisa Ugani katika Halmashauri 140 hapa nchini na kuagiza pikipiki hizo kutumika kwa malengo yaliokusudiwa ambayo ni kuwahudumia wafugaji katika maeneo yao na si vinginevyo.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mashimba Ndaki amesema amesema kikao kazi hicho kinalenga kupata namna bora itayosaidia kuongeza tija, kipato na kuongeza ajira katika sekta ya mifugo nchini.
Aidha amesema kutokana na hali ya ukame hapa nchini tayari baadhi ya maeneo yamekabiliwa na upungufu wa malisho ya mifugo na hivyo kupelekea kufa kwa mifugo ambapo Jumla ya Ng’ombe 69751, mbuzi 11024, kondoo 15742 na Punda 1680 zimekufa.
Katika kukabiliana na hali hiyo Waziri Ndaki amesema tayari wamezungumza na mamlaka za mabonde ya maji ili kuruhurusu mifugo kupata maji katika maeneo ya mabonde hayo pamoja na kufanya mazungumzo na mamlaka za hifadhi mbalimbali kuruhusu mifugo kupata malisho ndani ya hifadhi ili kunusuru hali hiyo.
Mwisho
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Tamisemi, Mifugo pamoja na wahusika wa sekta ya mifugo nchini wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa (Tamisemi). Januari 17,2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Tamisemi, Mifugo pamoja na wahusika wa sekta ya mifugo nchini wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa (Tamisemi). Januari 17,2022.
Post a Comment