MIAKA 45 YA CCM: UWT MWANZA WAASWA KUSHIRIKI ZOEZI LA SENSA

Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi UWT mkoa wa Mwanza imeadhimisha sherehe za kutimiza miaka 45 tangu kuzaliwa kwa chama hicho.

Jumuiya hiyo imeadhimisha kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo uandikishaji wa wanachama kielektroniki, upandaji miti, uzinduzi wa jengo la kitega uchumi linalojengwa kata ya Pasiansi na uhamasishaji wa ulipaji ada kwa wanachama.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo kimkoa yaliyofanyika katika viwanja vya ofisi za CCM Wilaya ya Ilemela Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Ellen Bogohe amewataka wanachama wa jumuiya hiyo kukiunga mkono chama chao kwa kuhakikisha wanajisajiri kielektroniki na kulipa ada.

Bogohe amewaasa wanachama kuwa na upendo na mshikamano hasa katika kipindi hiki ambacho kuna uchaguzi wa nafasi za wanawake katika chama sanjari na kuwaunga mkono wagombea wanawake wenye uwezo watakaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali.

"Pamoja na kusheherekea miaka 45 ya chama chetu, Mwaka huu tuna uchaguzi, Kina mama jitokezeni mgombee, Hakuna nafasi ya mwanaume, Kila mwanamke mwenye uwezo kipenga kikishapigwa ajitokeze kugombea na sisi wanawake wajibu wetu kumuunga mkono mwanamke mwenzetu" Alisema

Amewaasa wanachama hao kujitokeza kuhesabiwa pindi zoezi la Sensa litakapoanza na kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum nao wanahusishwa katika zoezi hilo.

Aidha Bogohe amempongeza Mwenyekiti wa Chama hicho ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan kwa kazi nzuri anazozifanya katika kuwatumikia wananchi sambamba na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula. 

Kwa upande wake mwenyekiti wa jumuiya hiyo wilaya ya Ilemela Bi Salome Kipondya amefafanua kuwa jumuiya yake katika kipindi kifupi cha mwaka huu imefanikiwa kusajili wanachama wapya zaidi ya mia mbili pamoja na kuanzisha mradi wa nyumba ya biashara inayojengwa katika kiwanja namba 127 kitalu ‘A’ Pasiansi.

"Nawaomba wanachama na viongozi tushirikiane kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo unakamilika"Amesema Mwenyekiti


Naye katibu wa jumuiya hiyo kutoka kata ya Nyakato Bi Zuhura Mohamed amemshukuru mwenyekiti huyo na kamati yake ya utekelezaji kwa namna wanavyoshirikiana na viongozi wa ngazi za chini katika kudumisha uhai wa jumuiya yao na kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayosaidia jumuiya hiyo kusongambele pamoja na kuwataka wanachama wengine kuunga mkono juhudi hizo za viongozi.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya miaka 45 ya Chama cha Mapinduzi CCM "CCM imara shiriki uchaguzi kwa uadilifu".

Mwisho.

Post a Comment

Previous Post Next Post