MWANAFUNZI WA CHUO AJINYONGA KISA SHILINGI 200



Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Udaktari Kilichopo Katika Mji wa Kitale Nchini Kenya, Diana Moraa mwenye umri wa miaka 25 amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia tai ya kuvaa shingoni.

Akithibitisha tukio hilo Afisa Mkuu wa Kitengo cha Polisi wa Kwanza (OCPD) James Odero amesema kuwa tukio hilo limetokea jana Jumatano Januari 26,2022 ambapo mwili wa marehemu ulikutwa katika chumba cha kulala cha wazazi wake huko kijiji cha Maziwa Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia Nchini Kenya.

OCPD Odero amesema kuwa marehemu ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa uuguzi katika chuo cha udaktari cha eneo hilo inadaiwa alimwomba babake Shilingi mia mbili (200) ya kenya (4000tsh)
  alizotaka kutumia katika mgahawa wa mtandao.

Ameongeza kuwa tayari wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo na mwili wa marehemu umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti.

kwa upande wa Mama mzazi wa Diana, Beatrice Adema amesema kuwa bintiye aliondoka nyumbani baada ya kupiga simu kwa mtu akitumia simu ya babake.

“Alirudi nyumbani mwendo wa saa tisa alfajiri na kwenda moja kwa moja chumbani kwake, Sikumsumbua sana aliporudi nyumbani kwa sababu nilikuwa na shughuli nyingi jikoni"

Aliongeza: "Hakuwa ametoka chumbani kufikia saa 3 usiku na tukawa na mashaka. Tuligonga mlango wake lakini hakukuwa na majibu."

Shimei Nyakeriga, ambaye ni baba mzazi wa marehemu alisema walimjulisha mjumbe wa Nyumba Kumi ambaye aliwasaidia kuingia ndani ya chumba hicho na kukuta mwili wa Diana ukining'inia kwenye paa ukiwa na tai ya shingoni.

"Hatujui ni kwa nini binti yangu alijiua. Hakukuwa na dalili yoyote kwamba alikuwa matatani. Hakuwa hata kulalamika kuhusu chochote," alisema.

Mwisho


Post a Comment

Previous Post Next Post