PICHA: MAKAMU WA RAIS AWAFARIJI WAFIWA

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiambatana na mkewe mama Mbonimpaye Mpango leo tarehe 24 Januari 2022 wametembelea na kutoa pole kwa familia ya mwanasiasa mkongwe mzee John Alfonso Nchimbi aliyefariki jumapili tarehe 23 Januari 2022 katika hospitali ya JKCI Jijini Dar es salaam.

Akiwa Tabata nyumbani kwa marehemu, Makamu wa Rais amempa pole mke wa marehemu Bi. Selva Nchimbi ,mtoto wa marehemu Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi pamoja na ndugu, jamaa na marafiki waliojitokeza katika msiba huo. Makamu wa Rais amewaomba wanafamilia pamoja na waombolezaji kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu na kuendelea kumuombea marehemu mzee John Nchimbi apumzike kwa Amani.

Mazishi ya mwanasiasa mkongwe mzee John Nchimbi yanatarajiwa kufanyika jumanne tarehe 25 Januari 2022 katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es salaam.

Aidha  Dkt. Philip Mpango  amemtembelea na kumpa pole Makamu wa Rais mstaafu Dkt Mohammed Gharib Bilal kufuatia kifo cha mama yake mzazi Bi. Safia Abeid kilichotokea tarehe 3 Januari 2022 na kuzikwa kijijini kwao Kaboje Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 4 Januari 2022.

Makamu wa Rais Dkt. Mpango amewapa pole wanafamilia na kuwaomba kuendelea kumuombea marehemu ili apumzike kwa Amani. Kwa upande wake Makamu wa Rais mstaafu Dkt. Bilal amemshukuru Makamu wa Rais kwa kuwapa faraja wanafamilia kufuatia msiba huo. Wakati huo huo Makamu wa Rais mstaafu Dkt Bilal amempa pole Dkt. Mpango kufuatia kifo cha kaka yake Askofu Mstaafu Dkt. Gerald Mpango kilichotokea tarehe 19 Januari 2022.

Mwisho

TAZAMA PICHA HAPA CHINI 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiweka saini katika kitabu cha maombolezo alipokwenda kutoa pole na kuifariji familia ya Mwanasiasa Mkongwe Marehemu John Alfonso Nchimbi ambaye ni baba mzazi wa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi  aliyefariki tarehe 23 Januari 2022 katika hospitali ya JKCI Jijini Dar es salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitoa pole kwa mama Selva Nchimbi ambaye ni mke wa marehemu John Alfonso Nchimbi aliyefariki tarehe 23 Januari 2022 Jijini Dar es salaam(katikati ni Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi). Januari 24,2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitoa pole kwa waombolezaji mbalimbali waliofika nyumbani kwa marehemu John Alfonso Nchimbi aliyefariki tarehe 23 Januari 2022 Jijini Dar es salaam.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitoa pole kwa Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohammed Gharib Bilal pamoja na familia yake kufuatia kifo cha Mama yake Dkt. Bilal aliyefariki tarehe 3 Januari 2022 na kuzikwa tarehe 4 Januari 2022 kijiji cha Kiboje mkoa wa Kusini Unguja .

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango pamoja na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakiwa katika picha ya pamoja na familia ya Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohammed Gharib Bilal alipofika kutoa pole kufuatia kifo cha Mama yake Dkt. Bilal aliyefariki tarehe 3 Januari 2022 na kuzikwa tarehe 4 Januari 2022 kijiji cha Kiboje mkoa wa Kusini Unguja.

Post a Comment

Previous Post Next Post