SIMBA WAAMBUKIZWA CORONA NA WAHUDUMU WA MBUNGA

 


Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini wamesema simba watatu na puma wawili waliopatikana na maambukizi ya virusi vya Corona waliambukizwa na wafanyakazi wa mbuga moja ya wanyamapori nchini humo.

Katika ripoti yao, wanasayansi hao wamesema simba na puma ambao wanatoka katika jamii ya paka wakubwa na ambao wamefungiwa sehemu kubwa, wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 kutoka kwa wanadamu.

Utafiti wa wanasayansi hao umesema kuwa, wanyamapori hao wa mbuga moja ya binafsi mjini Johannesburg waliambukizwa virusi vya Corona mwaka jana na wahudumu ambao walikuwa wanawashughulikia.

Profesa Marietjie Venter, mhadhiri wa taaluma ya virusi katika Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini amesema, kirusi cha Corona kinachofahamika kitaalamu kama SARS-CoV-2 ambacho walipatikana nacho wahudumu wa mbuga hiyo, ndicho kilichopatikana kwenye sampuli za simba na puma hao.

Wanasayansi hao wa Afrika Kusini waliamua kufanya utafiti huo baada ya kuona wanyama mwitu hao katika hifadhi hiyo ya kibinafsi wanasumbuliwa na matatizo ya kupumua, kutokwa na kamasi na kikohozi kikavu.

Utafiti huo umebainisha kuwa, wafanyakazi 12 wa mbuga hiyo walifanyiwa vipimo vya Corona, na matokeo yakaonyesha kuwa watano miongoni mwao walikuwa wameambukizwa; na hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa wao ndio waliambukiza wanyamapori hao.

Post a Comment

Previous Post Next Post