Shirika la umeme Tanzania TANESCO limewatoa hofu wateja wake kuhusu hali ya upatikanaji umeme nchini wakati wa uboreshaji wa mfumo wa gesi asilia kwenye visima vya gesi vya TPDC(Tanzania Petroleum Development Company) na PAET(Pan African Energy Tanzania) kama yalivyotangazwa kuanza tarehe 1 hadi 10 mwezi huu.
Akifafanua kuhusu matengenezo hayo leo Januari 30,2022 wakati wa ziara aliyoifanya na waandishi wa habari kwenye kituo cha kupoza umeme cha kunduchi jijini Dar es salaam Maharage amesema nchi haitakua gizani na kwamba hakuna maeneo yatakayoathirika kwa siku zote kumi mfululizo kwa kukosa umeme.
‘‘Visima vile vya gesi asilia si vya TANESCO ni vya TPDC, SONGAS na PAET sisi ni wateja tunaochukua gesi kutoka kwao na ili wao watupatie nishati hiyo zaidi ni lazima kufanya maboresho ndani ya siku hizo 10 tulizozitangaza, hakuna eneo litaathirika zaidi ya siku 3 kwa kukosa umeme ndani ya siku hizo kumi za kupisha matengenezo na tayari tumeshatoa ratiba kwa maeneo yote yatakayoathirika kwa kila mikoa husika nchi nzima.’’amefafanua Maharage.
Aidha amesema sambamba na matengenezo ya visima hivyo Shirika litaendelea na maboresho yake na matengenezo mbalimbali kwenye miundombinu yake ndani ya muda wa siku 10 katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha matengenezo yatakapokamilika huduma ya umeme inarejea katika hali yake ya kawaida.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema kazi ya kuongeza uwezo wa kupokea na kupoza umeme katika kituo cha kunduchi kilichoko eneo la Salasala jijini Dar es salaam iko ukingoni na tayari transforma mpya yenye ukubwa wa MVA 195 imekamilika kufungwa.
‘‘Transforma hii inategemewa kuwashwa ili kuanza kutumika wakati wa kipindi cha matengenezo ya visima vya gesi na umeme kama nilivyozungumza wiki ya jana’’ amesema Maharage.
Akieleza kwa undani faida za transforma hiyo kwa wateja wanaohudumiwa na kituo hicho Meneja mkoa wa Kinondoni kaskazini Mhandisi Regina Mvungi amesema transforma hiyo itasaidia kuondoa matatizo ya umeme kucheza, kuwa mdogo na kuboresha hali ya upatikanaji umeme kuwa ya kutabirika na ya uhakika.
Post a Comment