Serikali ya Tanzania imepokea dozi Laki 8 (800,000) za chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm kutoka Serikali ya watu wa China ambazo zitatumika kuchanja wananchi Laki 4 (400,000).
akizungumza mbele ya waandishi wa habari wakati wa hafla ya kupokea chanjo hizo iliyofanyika leo Jumatano Januari 26,2022 Jijini Dar es salaam,Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa hadi sasa Tanzania imepokea jumla ya dozi 8,821,210 zikijumuisha aina ya Sinopharm,Janssen,Moderna na Pfizer ambazo zinatosha kuchanja jumla ya watanzania 5,082,380.
Waziri Ummy amebainisha kuwa kuwa hadi sasa jumla ya watu 1,922,019 wamechanja ambao ni sawa na asilimia 3.3 pekee ya watanzania na kuongeza kuwa mpaka kufika tarehe 23 Januari,2022 jumla ya watu 33,000 wamethibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO-19 na watu 781 wamepoteza maisha.
Amesema kuwa asilimia 95 ya watu waliolazwa katika hospitali mbalimbali nchini kati ya kipindi cha Septemba, 2021 hadi Januari 23, 2022 walikuwa hawajapata chanjo ya UVIKO-19 na watu waliolazwa ni 3,147 huku kati ya hao 2,990 walikuwa ni ambao hawajachanja ambapo kipindi hicho vimetokea vifo 76 na 73 kati yake walikuwa hawajachanja.
"Waliokuwa mahututi {ICU} Januari 23 pekee walikuwa 31 na kati yao 30 walikuwa hawajachanja,kwa hiyo ni vizuri watu wapime katika hili, waliopata chanjo si wengi kama waliopata" Amesema Waziri Ummy
Aidha amemuagiza Mganga Mkuu wa Serikali kutoa takwimu za UVIKO-19 kila wiki ili kuongeza chachu kwa wananchi kupata chanjo kwa hiyari na kuongeza kuwa chanjo zimethibitishwa ubora na usalama na kwamba tangu zimeanza kutolewa nchini hakuna kisa chochote kilichoripotiwa mtu kupata madhara.
Amewahimiza Watanzania kuepuka matumizi holela ya dawa za 'antibiotics' kwani zinaweza kuzua janga jingine la usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya magonjwa. Amewasihi kufika vituo vya kutolea huduma za afya kupima kwa kuwa si kila homa au mafua ni UVIKO - 19
Kwa niaba ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassani Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya China kwa kuwezesha upatikanaji wa chanjo ikiwa ni awamu ya pili kwa chanjo za aina ya Sinopharm awamu ya kwanza ilipokea jumla ya dozi 500,00 ambazo zilitumika kuchanja wananchi 250,000.
Mwisho
Post a Comment