Serikali imekuja na suluhisho katika kukabiliana na changamoto za ukame uliosababisha vifo vingi vya mifugo kwa kutumia Sh bilioni 130 ili kuchimba visima, kukarabati na kujenga mabwawa ikianza na maeneo yaliyoathirika zaidi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega alieleza mkakati huo wa Serikali Januari 14,2022 wakati alipofanya ziara Wilaya ya Kiteto,Mkoani Manyara ili kuwapa pole kwa kufiwa na ng'ombe 1,874 kati ya Septemba 2020 hadi Januari mwaka huu.
"Serikali ya Mama Samia ni sikivu na inawajali wananchi wake, imenituma kuja kuwapa pole kwa kufiwa na ng'ombe wengi waliokufa kutokana na ukame kutokana na kukosa maji na malisho" alisema.
Aidha Mhe. Ulega baada ya kushuhudia mizoga ya ng'ombe katika kijiji cha Makame kata ya Makame akiwa katika mikutano ya hadhara kwenye kijiji cha Makame na Ndede alisema, Serikali inawapa Pole lakini imekuja na suluhisho la kukabiliana na ukame huo kwa kuchimba visima na mabwawa kwa ajili ya kunywesha mifugo.
Katika kuhakikisha wafugaji wanaondokana na vifo vingi vya mifugo na wanakabiliana na uhaba wa mifugo, Serikali itasambaza nyasi za malisho kwa mifugo kwa ajili ya wafugaji kuzipanda, kuvuna na kuhifadhi ili kuzitumia wakati wa ukame na msimu kama huu.
Katika kukabiliana na ukame huo, pia aliwataka wafugaji Kiteto na Tanzania kwa ujumla, kuacha kufuga mifugo kwa mazoea, wanatakiwa kuanza kupunguza mifugo yao kwa kuuza ili kujenga nyumba bora, kusomesha watoto na kuboresha mifugo inayobaki na kuuza sokoni ikiwa bora.
Mhe.Ulega alisema, wafugaji wanatakiwa kuitikia wito wa Serikali wa kuweka hereni kwenye masikio ya ng'ombe kwa lengo la kuweka alama ili badae kuzikatia bima ili zikifa waweze kulipwa na pia wakopesheke na taasisi za kifedha kuliko ilivyo sasa.
Naye Mbunge wa Kiteto, Edward Ole Lekaite (CCM) alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Shilingi bilioni 130 kwa Wizara ya Maji kwa ajili ya kununua mtambo mmoja wa kuchimba visima, mabwawa na malambo katika mikoa yote nchini na akaomba mitambo ikifika mkoani kwake kutokana na sababu ya ukame apewe kipaumbele.
Mhe. Lekaite alisema kutokana na changamoto ya ukame Wilaya yake ambayo imeua mifugo mingi inaomba mtambo wa kuchimba mabawa ukifika mkoani basi Wilaya yake iwe ya kwanza kupewa.
Akizungumzia vifo vya mifugo, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Afya kutoka Wizara ya Mifugona Uvuvi, Dk Vayan Laizer alisema vifo hivyo vinatokea sababu ya uhaba wa maji hivyo ng'ombe wanapokula majani mwituni na kukosa maji miili yao inakuwa na kinga kidogo na hivyo wanashindwa kujikinga na maradhi kutokana na sumu kubaki mwilini.
Naye Kaimu Mkurugenzi Sekta ya Afya Wilaya ya Kiteto, Dk Lunonu Sigalla wakati akitoa taarifa ya athari za ukame wilayani humo alisema kati ya Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu ngombe 1874 kutokana na ukame na waliobaki wamedhoofu sana kutokana na changamoto hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto,Bw. Mbaraka Batenga alisema uboreshaji wa miundombinu ya mifugo unatakiwa kwa lengo la kufungamanisha na miradi ya ujenzi wa shule sikizi zaidi ya 47 zilizojengwa katika wilaya hiyo na hivyo kuzuia kuhama hama wafugaji hao.
Mwisho
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiangalia ng'ombe aliyekufa kwa athari ya ukame kwenye kata ya Makame Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, akiambatana na Mbunge wa Kiteto Mhe. Edward Lekaita(wa kwanza kutoka kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Bw. Mbarak Batenga, (wa pili kutoka kushoto), viongozi wa chama, wafugaji na watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Januari 14,2022Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiongea na watendaji wa Wilaya ya Kiteto mara baada ya kuwasili Wilayani humo kuona athari ya ukame kwa wafugaji, kukusanya mawazo ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hizo Januari 14, 2022. Kulia ni Mbuge wa Kiteto Bw. Edward Ole Lekaita na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Bw. Mbarak Batenga.
Baadhi ya wafugaji wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo kwa Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (hayupo pichani) mara baada ya kufika katika kijiji cha Makame Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara wakati wa ziara yake Wilayani humo kuona athari ya ukame kwa wafugaji na kukusanya mawazo ya pamoja kukabiliana na changamoto hizo Januari 14,2022
Post a Comment