WATU WATANO WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA WANAWAKE WATATU MWANZA

Na Samir Salum

Watu watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya wanawake watatu wa familia moja wakazi wa mtaa wa Mecco Kusini jijini Mwanza.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu January 24,2022 Kamanda wa polisi mkoani Mwanza Ramadhani Ng’anzi amesema  chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa kibiashara.

Watu hao wa familia moja ambao ni Marry Charles mwenye umri wa miaka 42, Jenifa Fred mwenye umri wa miaka 22  ambaye ni mtoto wa marehemu Marry, pamoja na Monica Jonas mwenye umri wa miaka 19 ambae ni mfanyakazi wao wa ndani  waliuawa mnamo January 18,2022 kwa kukatwa mapanga na miili yao kutupwa kando ya mto uliopo Mtaa wa Mecco kusini, Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza.


Kamanda  Ng’anzi amesema kuwa marehemu Mary Charles alikuwa akijishughulisha na biashara ya kuuza nafaka akishirikiana na watuhumiwa wawili ambao ni mke na mume kuagiza mzigo wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

“Inadaiwa mara ya mwisho marehemu alimpa mmoja wa watuhumiwa kiasi cha fedha ambacho hakijajulikana kwa ajili ya kumuagizia mzigo, matokeo yake mzigo haukuletewa na katika kudaiana ndipo mtuhumiwa huyo wa kwanza akishirikiana na wenzake aliweza kwenda kufanya mauaji hayo,” amesema Kamanda Ng’anzi.

VIDEO: WANAWAKE WATATU WAUAWA MWANZA

Amesema kuwa watuhumiwa hao walikutwa na silaha aina ya panga iliyotumika kwenye mauaji hayo ambayo ipo chini ya uangalizi wa jeshi la polisi.

Marehemu Marry ameacha mtoto wa mwaka mmoja na binti yake Jenifa ameacha mtoto wa mwezi mmoja.

Watoto wa marehemu wapo chini ya uangalizi maalumu huku Miili ya marehemu ikizikwa kijijini kwao Bomani wilaya Sengerema usiku wa Januari 21, 2022.

Mwisho

Msikilize Kamanda wa NG'ANZI HAPA👇

Post a Comment

Previous Post Next Post