Na.Angela Msimbira TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa akerwa vikali na mikwaruzano inayoendelea kwa watumishi wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) hali ambayo inaharibu taswira na muonekano wa Taasisi hiyo muhimu kwa jamii.
Akiongea na Menejimenti na watumishi wa TARURA leo, Mtumba Jijini Dodoma Waziri Bashungwa amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia. Suluhu Hassani anamategemeo makubwa na Taasisi hiyo ambayo ndio kiungo muhimu katika kutatua kero za wananchi.
“Nimeifahamu migogoro ya TARURA kupitia kwenye vyombo vya habari, mikwaruzano yenu ya ndani inaonesha uhalisia wa migogoro iliyopo, Jambo hili halijanipendeza, hivyo mnanilazimisha kwenye majukumu yangu ya kwanza niwamulike kiundani, kwa hilo siko tayari kuwa na Taasisi ambayo badala ya kunisaidia nimsaidie Rais katika kutatua changamoto za wananchi, yenyewe inakuwa na migongano ya kila wakati kugombana badala ya kukaa ndani na kujipanga ili kuweza kutatua changamoto za wananchi” amesema Waziri Bashungwa
Waziri Bashungwa amesema ataingalia taasisi hiyo kwa jicho la karibu ili kuweza kuhakikisha inatimiza majukumu yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi, na kusisitiza kuwa hatasita kuwachukulia hatua watumishi au viongozi wachache wanaotaka kuirudisha nyuma taasisi hiyo.
Amesema kuwa si maadili na ni kinyume na utaratibu wa kutoa siri za Taasisi au za Serikali zinatoka nje kinyume na utaratibu, kwenye hili TARURA mmeonyesha mfano mbaya kwa kuwa hali ya mikwaruzano ndani ya menejimenti inakwanza utendaji kazi wa Taasisi hiyo
Amesema hatakuwa tayari kwa mtumishi yeyote anayekwamisha dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ya watu wachache wanaotaka kurudisha nyuma utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hii Muhimu kwa jamii.
Aidha, amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhakikisha anafuatilia na kuchambua mgogoro huo na kuwaasilisha taaarifa ili kuchukua hatua stahiki.
Post a Comment