WAZIRI BITEKO ATAJA MAFANIKIO KUANZISHWA KAMPUNI YA MADINI YA TWIGA..MAKUSANYO YAFIKIA BIL 528

 


Na WM Kahama-Shinyanga

Serikali imeeleza mafanikio yaliyopatikana kutokana na kuanzishwa kwa kampuni ya Madini ya Twiga (Twiga Minerals Corporation Limited) inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya  Uchimbaji madini ya  Barrick Gold. 

Kabla ya mwaka 2015 mapato ya serikali yaliyokuwa yanatokana na madini yalikuwa hayazidi Shilingi Bilioni 115 ambapo kwa Mwaka wa Fedha  2020/2021 pekee serikali imefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 528.

Waziri wa Madini  Dkt. Doto Biteko ameyasema hayo leo tarehe 25 Januari 2022, katika Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga  wakati akizungumza na ujumbe wa kampuni ya Barrick ulioongozwa na Rais na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo ya Barrick Duniani Dkt Mark Bristow.

Waziri Biteko amesema kuwa Kampuni ya Barrick inamiliki asilimia 84 za hisa huku Serikali ya Tanzania ikiwa inamiliki asilimia 16 jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa Pato la serikali linalotokana  Shughuli  za madini.

Kampuni ya Barrick ndio kampuni ya kwanza kuingia ubia na kampuni ya serikali na baadaye zikafuata kampuni zingine nne kusaini mikataba yenye thamani  dola za  Mrekani  milioni 763 ambapo kampuni tatu  za uchimbaji madini ni kutoka Australia na moja kutoka Uingereza. 

Kampuni zilizotiliana saini na serikali na kuunda kampuni za ubia ni Strandline Resources Ltd na kuunda Kampuni ya Ubia ya Nyati Minerals Sands Ltd itakayokuwa inachimba mchanga Fungoni wilayani ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam na Kampuni ya Black Rock Mining Ltd na kuunda Kampuni ya Ubia ya Faru Graphite Corporation iliyopo wilayani Ulanga mkoani Morogoro kwa ajili ya kuchimba madini ya kinywe.

Mikataba mingine iliyosainiwa ni kati ya serikali na Kampuni ya Nyanzaga na kuunda Kampuni ya Ubia ya Sotta Mining Corporation Ltd iliyopo Sengerema mkoani Mwanza kwa ajili ya kuchimba dhahabu na Kampuni ya Petra Diamond Ltd na kuunda Kampuni ya Ubia ya Williamson Diamond Ltd kwa ajili ya kuchimba madini ya almasi Mwadui mkoani Shinyanga.

Naye,  Rais na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo ya Barrick Duniani Dkt Mark Bristow amesema ubia baina ya kampuni yale na serikali umeongeza tija ya uzalishaji wa madini.


Amesema kuwa mgodi umetoa fursa za ajira kwa wazawa ambapo asilimia 96 ya wafanyakazi ni watanzania huku asilimia 41 wakiwa wanatoka katika vijiji vinavyozunguka mgodi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Sophia Mjema amesema kuwa uongozi wa Mkoa na Wilaya zote zitaendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo ili kuongeza ufanisi na tija katika upatikanaji wa madini.

Kadhalika, Waziri Biteko akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kakola Wilayani Kahama amewatoa hofu wananchi wenye kero mbalimbali ikiwa ni pamoja na zile zinazohusu madai ya fidia ya ardhi, ambapo amesisitiza kuwa serikali inafuatilia kwa karibu kuhakikisha wanapata stahiki zao.

MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post