WATU 120 WAFARIKI DUNIA, MAELFU WAKOSA MAKAZI KUTOKANA NA KIMBUNGA BATSIRAI



Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na Kimbunga cha Batsirai nchini Madagascar imeongezeka na kufikia watu 120.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana Ijumaa Februari 11,2022 na taasisi ya kushughulikia maafa ya nchi hiyo kupitia Vyombo vya habari imesema kuwa idadi ya wahanga imeongezeka baada ya nyumba zao kuporomoka katika mji wa Ambalavao, ulioko umbali wa takriban kilomita 161 kusini mwa mji mkuu, Antananarivo.

Taasisi hiyo imesema kuwa hadi kufikia jana ijumaa wahanga waliongezeka kutoka 92 hadi 120.

Imeongeza kuwa kimbunga hicho kimewaacha zaidi ya watu 124,000 kukosa makazi baada ya nyumba zao kuharibiwa na wengine 30,000 wamelazimika kuyahama makazi yao na kupiga kambi katika maeneo 108.



Kimbunga Batsirai kilitokea nchini humo Jumamosi Februari 05, 2022 ambapo kilifika eneo la Mananjary, kikiwa na upepo unaokwenda kwa kasi ya maili 103 kwa saa ambapo kikisababisha maafa ikiemo kung'oa miti, kuharibu majengo na kuwafanya maelfu ya watu kukosa makazi yao.

Kabla ya kufika kimbunga hicho, Ofisi ya Taifa ya Hali ya Hewa ya Madagascar ilitangaza kuwa mvua kubwa itasababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Aidha Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) lilitabiri kuwa kimbunga Batsirai kinatazamiwa kusababisha upepo mkali na mvua kubwa katika maeneo ya pwani ya Madagascar.

Kimbunga Batsirai kimeikumba Madagascar ikiwa ni chini ya wiki mbili baada ya kimbunga kingine kiitwacho Ana kusababisha vifo vya watu 58 na wengine zaidi ya 130,000 kupoteza makazi yao kisiwani Madagascar.

Vimbunga vimekuwa vikiikumbwa Madagascar mara kwa mara ambavyo mbali na kusababisha maafa makubwa ya roho na mali, Maelfu ya watu wamekuwa wakiacha bila makazi, huku miundombinu na mifumo ya mawasiliano ikiharibiwa vibaya.

Post a Comment

Previous Post Next Post