ZAIDI 60% YA WATANZANIA WANATUMIA TIBA ASILI KUTIBU MAGONJWA MBALIMBALI


Na WAF- DODOMA 

Kaimu Mkurugenzi wa huduma  za  tiba Wizara ya Afya Dkt. Caroline Damiani amesema, zaidi ya asilimia 60% ya Watanzania wanatumia tiba asili ili kujitibu dhidi ya magonjwa mbalimbali kabla ya kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya au baada ya kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma za kisasa. 

Ameyasema hayo leo Februari 17, 2022 Jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa Waganga wa tiba asili yenye lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto na mikakati mbalimbali ya kuikuza taaluma ya tiba asili na tiba mbadala ili iendelee kuwanufaisha Watanzania. 

"Watanzania zaidi ya asilimia 60 kwa wakati mmoja ama mwingine wanapata tiba asili kwaajili ya maradhi mbalimbali kabla ya kwenda katika vituo vya kutolea huduma au baada ya kwenda katika vituo ama hospitali zetu zinazotoa huduma za kisasa" Amesema Dkt. Caroline. 

Amesema, dhima kuu ya mafunzo haya ni kuhakikisha dawa zinazotengenezwa na Wataalamu zinakuwa bora kuanzia katika hatua ya uoteshaji, uvunaji, utengenezaji, uhifadhi mpaka hatua ya kumfikia mlaji ili isilete madhara kwenye afya ya mtumiaji. 

Dkt. Caroline amesema, mpaka sasa Wizara ya Afya kupitia Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala limefanikiwa kusajili dawa za tiba asili 73, huku akiweka wazi kuwa kati ya dawa hizo 73, dawa 20 zilileta mafanikio makubwa sana katika kipindi cha mapambano dhidi ya UVIKO-19. 

Aidha, Dkt. Carolin amesema, wameweza kujadili njia bora ya kuhakikisha dawa za tiba asili ziweze kupatikana kwa urahisi zaidi popote nchini na nje ya nchi ili kuwanufaisha Wananchi na kunufaisha Taifa kwa kupata fedha za kigeni baada ya kuziuza nje ya nchi. 



Mbali na hayo, Dkt. Caroline amewataka kuungana na kuimarisha ushirikiano baina yao ili kupata nguvu ya pamoja katika jitihada za kuikuza taaluma ya tiba asili nchini. 

Sambamba na hilo, amewataka kuanzisha viwanda vya kutosha vitavyozalisha dawa za tiba asili, hali itayosaidia kuongeza upatikanaji wa dawa hizo katika maeneo mbalimbali nchini na kuwanufaisha wananchi. 

Hata, hivyo Dkt. Caroline ametoa wito kwa Waganga wa tiba asili kuzingatia maelekezo na maagizo ya Wizara ili kuweza kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba taaluma hiyo. 

"Tunatoa wito kwa watengeneza dawa wote nchini waweze kuzingatia maelekezo na maagizo ya Wizara ya Afya ili tuweze kushirikiana kwa pamoja kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba taaluma hiyo" Amesema Dkt. Caroline 

Serikali inathamini mchango mkubwa wa taaluma ya tiba asili na tiba mbadala na itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Waganga wa tiba asili nchini katika kuhudumia afya za wananchi dhidi ya magonjwa. Amesema 

Naye Mwakilishi wa Waganga wa tiba asili na tiba mbadala na Mbunge wa Lushoto, Shaban Omary Shekilindi ameipongeza Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Tiba asili na Tiba mbadala kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuwajenga na kukumbushana Sheria na taratibu za taaluma ya tiba asili nchini. 

Pamoja na hayo Shekilindi ameiomba Serikali kuendelea kuiinua taaluma ya tiba asili kwani Waganga wengi vipato vyao ni vidogo kukidhi malengo yao ya kuwahudumia wananchi, huku akisisitiza kuwa, endapo Serikali itawekeza zaidi kwenye tiba asili, inaweza kuliingizia taifa pato kubwa hata kuliko madini 

Mwisho.

Post a Comment

Previous Post Next Post