Furaha Samweli Ligate (26) mkazi wa kijiji cha Unyangala wilaya ya Makete mkoani Njombe amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mara mbili mtoto mwenye umri wa miaka 15 aliyekuwa amehitimu darasa la 7 mwaka 2021 akisubiri kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wa 2022
Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya wilaya ya Makete Machi 14, 2022 mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama hiyo Mh.Ivan Msacky na mwendesha mashitaka Inspekta Msaidizi wa Polisi (Asistant Inspector) Benstad Samson Mwoshe
Imeelezwa kuwa bila hiyari mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo la ubakaji Desemba 24, 2021 majira ya saa 12 jioni na kurudia tena Desemba 25, 2021 kinyume na kifungu cha 130 (1)(2)(e) kikisomeka pamoja na Kifungu cha 131(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019
Mshtakiwa huyo anadaiwa kumwita chumbani kwake mtoto huyo ambaye anamwita mshtakiwa mjomba na kumbaka kisha kumtishia kumdhuru endapo angesema kwa mtu yeyote kama amefanyiwa kitendo hicho.
Mtoto huyo alishindwa kuvumilia na kutoa taarifa ambapo mshtakiwa alikamatwa na hatua zikachukuliwa hadi kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani na pia mtoto huyo alipofikishwa hospitali kwa uchunguzi iliguundulika kuwa ameingiliwa kimwili na ni mjamzito
Mwendesha mashitaka wa serikali Inspekta Msaidizi wa Polisi Benstard Mwoshe ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine.
Kwani kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha kikatili na kimemuathiri mtoto pamoja na kukatisha ndoto zake za kimasomo
Akizungumza mahakamani hapo kabla ya hukumu kutolewa mshtakiwa huyo ameiomba mahakama hiyo imuonee huruma na kumpunguzia adhabu kwa kuwa ana familia inayomtegemea ikiwemo mama yake mzazi ambaye ni mzee pamoja na watoto watatu ambao wanamtegemea na amewaacha bila utegemezi wake
Hakimu Mkazi Msacky amesema mahakama hiyo imezingatia maombi ya mshtakiwa ya kupunguziwa adhabu hivyo mahakama hiyo imemtia hatiani kwa kosa la ubakaji na kumhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani.
Post a Comment