Tovuti ya habari ya Iran, Nournews inayoonekana kuwa karibu na baraza kuu la usalama la taifa la nchi hiyo, iliripoti kuwa serikali imesitisha kwa upande mmoja mazungumzo na Saudi Arabia, ambayo yamekuwa yakiendelea mjini Baghdad
Iran imeamua kusitisha kwa muda mazungumzo yake ya siri yaliyofanywa na Baghdad yenye lengo la kupunguza mivutano ya miaka mingi na hasimu wake wa kikanda Saudi Arabia, chombo cha habari cha Iran chenye uhusiano na serikali kiliripoti Jumapili, siku moja baada ya Saudi Arabia kutekeleza kuwanyonga watu wengi katika historia yake ya sasa.
Tovuti ya habari ya Iran, Nournews inayoonekana kuwa karibu na baraza kuu la usalama la taifa la nchi hiyo, iliripoti kuwa serikali imesitisha kwa upande mmoja mazungumzo na Saudi Arabia, ambayo yamekuwa yakiendelea mjini Baghdad katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kwa lengo la kurejesha uhusiano wa kidiplomasia.
Awali waziri wa mambo ya nje wa Iraq, alisema kuwa duru ya tano ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa Saudi Arabia na Iran ingetarajiwa kuanza tena Jumatano.
Ripoti hiyo haikutoa sababu ya Iran kusitisha kwa muda mazungumzo, lakini inakuja baada ya Saudi Arabia kuwaua watu 81 waliopatikana na hatia ya uhalifu, kuanzia mauaji hadi uhusiano na makundi ya wanamgambo, kundi ambalo wanaharakati wanaamini lilijumuisha zaidi ya darzeni tatu za wa-shia.
Wa-shia ambao wanaishi hasa katika eneo la mashariki katika ufalme huo wenye utajiri wa mafuta, wamelalamika kwa muda mrefu kwamba wanatendewa kama raia wa daraja la pili. Hatua ya Saudi Arabia dhidi ya kuwanyonga wa-shia ilizua machafuko katika eneo hilo hapo awali.
Iran, nchi kubwa zaidi ya waislam wa madhehebu ya shia duniani, na Saudi Arabia yenye nguvu katika upande madhehebu ya wasunni, ilikata uhusiano wa kidiplomasia mwaka 2016, baada ya Saudi Arabia kumuua kiongozi maarufu wa kishia, aliyejulikana kama Nimr al-Nimr. Wa-Iran waliokuwa na hasira wanaopinga kitendo cha kunyongwa kwake, walivamia balozi mbili za kidiplomasia za Saudi Arabia nchini Iran, na kuchochea uhasama wa miaka mingi kati ya mataifa hayo.
Jumamosi jioni maandamano ya hapa na pale yalizuka miongoni mwa wa-shia katika ufalme wa karibu huko nchini Bahrain, kuhusiana na mauaji hayo ya watu wengi.
Post a Comment