MCHUNGAJI ALIEKUWA JAMBAZI SUGU, ASIMULIA YALIYOMKUTA NA ALIYOYAFANYA INAOGOPESHA..

Mchungaji ambaye amekiri kuhusika na ujambazi wa hali ya juu nchini Kenya wakati wa ujana wake miaka ya 90.

Rebecah alikuwa anaishi kijijini kwao kaunti ya Makueni hadi alipofikisha miaka 23 akaamua kutoka kwao kwenda mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Kulingana na Rebecah safari yake hiyo ilihusishwa kwa kiasi kikubwa na pilkapilka ya kutafuta riziki. Huo ulikuwa mwaka 1995 alipoanza kufanya kazi za kuajiriwa yaani vibarua vya hapa na pale.

''Nilipoingia Nairobi niliajiriwa vibarua mbalimbali. Lakini tangu zamani, sikuwa napendelea sana kuajiriwa kwa hio ilipofika mwaka 1997, nilianza biashara zangu mwenyewe. Nilikuwa nauza nguo, viatu nikawa nazunguka masoko mbalimbali ila biashara yangu ilikuwa katika soko kuu la Kawangware," anasimulia Rebecah.

Mwanadada huyo anasema alikuwa akijitahidi katika biashara yake kwa sababu ndio ilikuwa ikimpa kipato. Lakini kama ilivyo kwa biashara nyingine yoyote, kuna wakati alikumbana na misukosuko kutokana na ushindani mkali.

Hivyobasi, kutokana na hilo, alilazimika kutafuta njia mbadala ya kujitafutia riziki.

Ni katika pilkapilka hizo anasema kwamba alikutana na watu ambao ni 'wajanja' kutafuta hela.

Akimaanisha kwamba wakati yuko kwenye biashara zake sokoni, alikutana na watu ambao walikuwa wa genge la majambazi.


''Mwaka huo huo wa 1997 ndio niliamua kujiunga na genge la majambazi, tulianza tu kwa kubadilishana mawazo kuhusiana na jinsi ya kufanikiwa maishani na vile unavyoweza kuendesha biashara wakati mambo ni magumu. kwa hiyo nilijipata tumezoeana na hao watu ambao walinifumbua macho kwamba kuna biashara zingine haramu ambazo zingenipatia utajiri wa haraka bila kuchoka. Hivyo ndivyo nilivyojipata nikiwa ndani ya genge la wizi wa kimabavu," anasema Rebecah.''

Mwanadada huyo anaongeza kwamba kiu ya utajiri na kumbukumbu ya mahangaiko aliyokuwa nayo katika maisha yake kule kwao kijijini, ilikuwa kichocheo tosha cha yeye kujiunga na genge hilo.

''Nilianza kwa kuwa kwenye genge lililokuwa linawaibia watu vitu vya kawaida, mfano, vyombo vya kielektroniki, pesa, yaani wizi mdogo mdogo tu, lakini baada ya muda nilitoka kwenye genge hilo na kujiunga na kujiunga na genge jingine suku zaidi, hili ni genge lililokuwa linahusika na wizi wa kimabavu katika mashirika makubwa," anasimulia Rebecah.

Ila anasema kwamba mmojawapo ya sheria za kuingia kwenye genge hilo ilikuwa lazima angepata mafunzo mbali mbali na pia kusomeshwa kuhusiana na sheria zao.

Mwanadada huyo anasema miongoni mwa sheria hizo ilikuwa kwamba mtu akikamatwa atakubali kuwekewa lawama na na yeye pekee yake ndiye atakaye kuwa mashakani bila kutaja wenzake au kutoa nje siri za genge hilo liwe liwalo.

Mwanamke huyo anakumbuka jinsi walivyo husika na wizi wa kimabavu ambao ulitekelezwa kwa kutishia watu na bunduki hasa wakati walipofanya uhalifu katika baadhi ya benki.

Anasema kwamba kila operesheni ya uhalifu ilianza na mipango makhsusi ambayo kila mtu alikuwa anapewa majukumu yake vilivyo.

Yeye akiwa ni mwanamke katika genge lililokuwa na wanaume wengi, anasema majukumu yake yalikuwa pamoja na kuweka silaha hizo haramu na wakati mwingine alihusika kama mtu wa kwanza kuingia eneo la tukio katika hali yakuwafumba macho watu kabla ya genge kuvamia.

''Wakati huo nilikuwa mrembo zaidi na bado nilikuwa na umri mdogo kwa hiyo ningeingai eneo ambalo tumepanga kutekeleza wizi, nilikuwa nazungumza na wale wakuu wa pale kama njia ya kuwazubaisha na ghafla tunavamia, hakuna operesheni ya wizi ambayo ingefikisha dakika tano kabla ya kumalizika. Ni kitu kilichokuwa kinafanyika ghafla kwa sababu tayari ilikuwa inajulikana na hela ngapi tunaziiba kulingana na maelekezo ya hata wahusika wengine ambao ni wafanyikazi katika eneo la uhalifu" anakumbuka Rebecah.

Mwanadada huyo anasema kwamba kazi ya uhalifu ilimzungusha maeneo mbali mbali nchini Kenya.

Anakumbuka mwaka 1998 katika hali ya operesheni za uhalifu na wizi, baadhi ya hizo zilikuwa zinaripotiwa kwenye vyombo vya habari nchini Kenya.

Ila anasema kwamba majuto ni mjukuu kwani wengine wengi waliokuwa wanahusika, walipigwa risasi katika operesheni kadhaa na wakapoteza maisha yao.

''Hakuna kitu kibaya kama wizi, zile pesa unazipata. Ndio! lakini ukiangalia jinsi unazitumia ni kama zimelaaniwa. Kitu ambacho nimekisoma ni kuwa ningefaidika aje na hela ya wizi ilhali mimi sijazitolea jacho, sijui zimetoka wapi? kwa hiyo wakati mwingi hiyo hela ilikuwa ni ya raha tupu na kununua vitu ambazo havieleweki "Rebecah anakumbuka.

Mwanamke huyo anasema kwamba kama jambazi alikuwa na tabia ya kuhamahama kutoka nyumba mmoja hadi nyingine kwa kuhofia kwamba angejulikana.

Anakiri kuwa majambazi wengi huwa hawaishi sehemu mmoja kila wakati ila wanakuwa na nyumba katika pande tofauti tofauti na wanakuwa na tabia ya kuzunguka zunguka kila wakati.

Anataja maisha ya uhalifu kama yenye wasiwasi na kiza kikuu kila unapokuwa. Ila hajasahau mwezi wa saba mwaka 1998 walipokwenda kwa operesheni ya wizi, walikosa kufanikiwa baada ya mwenzao ambaye alikuwa amepewa jukumu la kutangulia kwenye eneo la uhalifu kufika pale na kuanza kupiga gumzo na watu na kusahau kwamba walikuwa katika mipango ya wizi.

Kulingana na Rebecah, mara nyingi aliwaza kuiwacha ile kazi lakini pesa ya haraka ilimsukuma zaidi na zaidi kutaka kutenda uhali.

Mwaka 1999 alikuwa bado kwenye operesheni za wiki kama kawaida wakati huo yeye ndiye alikuwa anaweka silaha za kazi.

Katika harakati hizo ilikuwa ni kana kwamba mambo yake yalikuwa yameanza kujulikana kwani watu hasa majirani walikuwa wanamshuku ila hawakuwa na namna ya kumgundua.

Vilevile, makachero waikuwa katika pilkapilka za kusaka wahalifu. Rebecah anasema kwamba wenzake walikuwa katika hali ya kujiandaa kwenda operesheni ya wizi ila alikuwa hajawapa silaha za kazi nyakati za jioni.

Akiwa katika eneo alilokuwa anaficha silaha hizo haramu, alikamatwa na makachero wanaofahamika kama 'Flying Squad,' wenzake katika genge hilo walifanikiwa kutoroka.

Alifunguliwa kesi ya wizi wa kimabavu na kufungwa gerezani kwa miaka 4 katika gereza la wanawake la Langata.

Maisha ya Rebecah yalibadilika akiwa gerezani. Alianza kujirudi na kujutia uhalifu aliotekeleza na akaanza maombi ya toba.

Anasema kwamba alianza kufwatilia mafundisho ya kidini hadi akajipata ameokoka akiwa gerezani.

Tamaa ya kuwa na uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu ilimsukuma hadi akaanza masomi ya kidini akiwa gerezani.

Alihitimu na kuanzisha utumishi wake kama mchungaji akiwa mfungwa katika gereza la Langata.

''Nilianza kuwa na shauku ya kutafuta Mungu kutokana na kuona kwamba ujanja wangu umefika mwisho. Nilikubali kuokoka kwani nilitamani kung'olewa mizizi ya wizi na mahangaiko mengi yalioandamana na uhalifu. Mwaka wa 2000 ndio wakati alianza kubadilika akiwa gerezani," anasema Rebecah.

Mwaka wa 2004 Rebecah alitoka gerezani ila hakurejelea maisha ya wizi tena. Aliendelea na huduma ya kuhubiri na kuwa mchungaji kamili.

Mama huyo anasema kwamba shauku yake kuu katika huduma ya kuwa mchungaji imekuwa sana katika kutoa nasaha hasa kwa vijana dhidi ya wizi.

Amekuwa akihusika sana na kazi za Kievanjelisti ambako huzunguka miji tofauti nchini kenya akitumia historia yake ya wizi wa kimabavu kuelimisha wengine.

Rebecah alithibitisha kuwa hapo awali kabla ya kukamatwa alikuwa amefunga ndoa na mmoja ya wanaume ambao walikuwa kwenye genge la majambazi.

Mama huyo anasema kwamba ilikuwa rahisi kwake kuwa na mahusiana na mtu ambaye walikuwa na upeo mmoja wa maisha.

Japo anakiri kuwa hata mumewe alibadilisha maisha yake kutoka kuwa jambazi, na wangali wako kwenye ndoa wakiwa ni watu tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

#ChanzoBBCSwahili





Post a Comment

Previous Post Next Post