MADIWANI BUCHOSA WAOMBA UCHUNGUZI ONGEZEKO LA WATOTO WANAOZALIWA NA VIRUSI VYA UKIMWI.

 NA OSCAR MIHAYO.

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Buchosa Mkoani Mwanza kwa pamoja wameazimia kuitaka Halmashauri hiyo kuchunguza na kuja na majibu ya kujitosheleza kutokana na kuibuka wimbi la watoto kuzaliwa na Virusi vya Ukimwi.



Akitoa maazimio hayo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hilo Maxmiliani Mkungu Diwani wa Katwe amesema ni hatari kuona licha ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujipambanua katika kuhakikisha uzazi salama kwa akina mama na watoto lakini bado kuna uzembe kwa watendaji kwenye kada hiyo.


“Tunataka majibu yakutosha ili kujua kama ni uzembe wa watendaji ama nini hasa kinasababisha watoto kuzaliwa na VVU wakati watalaam wapo na wanatakiwa kulinda Afya ya Mtoto hata pale inapotokea mama anamaambukizi,” amesema Mkungu.

Awali akitoa hoja hiyo Diwani Viti Maalumu Grace Mwabano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ukimwi amesema taarifa ya robo tatu ya mwaka inaonyesha watoto zaidi ya 84 wamezaliwa na Virusi vya Ukimwi.

Amesema hali inahuzunisha na hatua za haraka zinabidi zichukuliwe kwani licha watoto hao kuzaliwa na VVU lakini bado wanaoanza kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo ni wachache ukilinganisha na wahitaji.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Buchosa Irene Mkerebe amesema taarifa hiyo ameipokea na anaanza kuchunguza lakini taarifa aliyonayo ni kwamba watoto hawa sio wanaozaliwa na VVU bali wanazaliwa na akina mama wenye VVU.

“Nimepokea maagizo ya Baraza na naanza kulichunguza ili kama kweli tatizo hili lipo tuweze kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha wazazi wote wanaojifungulia kwenye Zahanati zetu na Vituo vya Afya wanakuwa salama wao na watoto wao”,amesema Irene.

Post a Comment

Previous Post Next Post