Huduma hizo zikiwemo upasuaji mkubwa wa magonjwa ya wakina mama,Figo na Saratani zitatolewa kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 17 - 21 June mwaka huu
Jopo la Madaktari hao limepokelewa na katibu tawala wa mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana ambae amempongeza Rais Samia kwa mpango huo unaolenga kuwasaidia wananchi kupata huduma za kibingwa katika maeneo yao.
Bwana Baladya ameongeza kuwa Madaktari hao wapatao 45 watasaidia kupatikana kwa huduma za kibingwa ikiwemo upasuaji mkubwa kwa magonjwa mbalimbali huku akiishukuru Wizara ya Afya kwa kufanikisha jambo hilo muhimu ambapo wananchi watapata huduma za kibingwa kwa gharama ndogo.
"Huduma zitawafikia wanachi huko waliko kwa gharama ndogo lakini mgonjwa atatakiwa kuchangia kiasi kidogo iwapo atahitajika kupata huduma zinginezo ikiwemo huduma ya vipimo, dawa na huduma za upasuaji",amesema Mtendaji huyo wa Mkoa
Aidha Balandya ametoa wito kwa wananchi wote wenye matatizo ya kiafya kuhudhuria kwenye hospitali hizo za Wilaya kuonana na kutibiwa na madaktari bingwa ambapo itawasaidia kupunguza gharama za kusafiri umbali mrefu nje ya Wilaya zao kufuata huduma za kibingwa.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Bi. Fideo Obimbo amesema lengo la ujio wa madaktari hao bingwa ni kuwafuata wagonjwa wale ambao hawana uwezo wa kufikia huduma za kibingwa na kampeni hiyo imelenga kufikia mikoa yote 26 ambapo kwa sasa wamefikia mikoa 20.
"Kampeni hii imekuwa na matokeo chanya ambapo mpaka sasa tumeshafikia wagonjwa 51471, miongoni mwao wagonjwa 6571 tuliweza kuwapatia huduma na wakalazwa katika hospitali hizo hizo za ngazi za chini",amesema Fideo.
Post a Comment