MABALOZI WANAOIWAKILISHA TANZANIA WATAKIWA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo, Kuwait, Israel ,Brazil na Urusi walipokwenda kumuaga Ikulu Chamwino Jijini Dodoma. Januari 26,2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo, Kuwait, Israel ,Brazil na Urusi walipokwenda kumuaga. Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma. Januari 26,2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo, Kuwait, Israel ,Brazil na Urusi walipokwenda kumuaga. Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma. Januari 26,2022.

*****

NA OMR-DODOMA

Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali wametakiwa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na manufaa kwa Tanzania. 

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Jumatano Januari 26,2022 Ikulu Chamwino Jijini Dodoma ambapo Makamu wa Rais amekutana na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo, Kuwait, Israel ,Brazil na Urusi.

Dkt Mpango amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa na imani waliopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuliwakilisha taifa kwenye nchi hizo. Makamu wa Rais amewasihi Mabalozi kwenda kufanya kazi kwa weledi na uzalendo kwa maslahi ya taifa.

Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi hivyo amewataka Mabalozi hao kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na manufaa kwa Tanzania.

Aidha amewaasa Mabalozi hao kutambua vipaumbele vya taifa ikiwa ni pamoja na kufahamu takwimu za msingi ikiwemo Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, Dira ya taifa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano zitakazochagiza katika kutafuta wawekezaji.

Amesema ni muhimu kwa Mabalozi hao kufanya jitihada za makusudi kuzifahamu vema nchi wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania ili kuweza kujifunza misingi ya ukuzaji wa uchumi wao na kuhamisha maarifa hayo kwa taifa la Tanzania. Amesema katika kutekeleza diplomasia ya uchumi Mabalozi hao wanapaswa kuongeza ushirikiano na vongozi wa sekta binafsi ili kuwavutia kuwekeza Tanzania.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka msisitizo katika kuleta mabadilizo katika uwekezaji pamoja na kuimarisha sekta ya viwanda hivyo amewasihi mabalozi hao kujielekeza katika kutafuta teknolojia rafiki zitakazosaidia katika kukuza na kuendeleza viwanda kulingana na mazingira ya hapa nchini.

Katika hatua nyingine Dkt Mpango amewaagiza Mabalozi hao Kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini pamoja na kutafuta fursa za ushirikiano hasa katika taasisi za utafiti na maendeleo. 

Amesema Mabalozi wanapaswa kutafuta fursa mbalimbali kwa nchi ya Tanzania  ikiwemo kuwavutia watalii na kuhakikisha wanashiriki katika mikutano mbalimbali itayowezesha kueleza mazuri ya Tanzania pamoja kuvutia wawekezaji.

Aidha amesema Mabalozi wanapaswa kuwaunganisha watanzania wanaoishi katika nchi wanazokwenda kuwakilisha ili kuwa na mawazo ya pamoja namna wanavyoweza kuwekeza hapa nchini na kurudisha ujuzi na maarifa walioyonayo nyumbani Tanzania.

Makamu wa Rais amewasihi Mabalozi hao kuwa na nidhamu ya matumizi ya pesa zinazopelekwa katika kuendesha Balozi hizo ili kuongeza tija ya uwakilishi katika vituo vyao.

Akishukuru kwa niaba ya mabalozi hao Balozi wa Tanzania nchini Brazil Prof. Adelardus Kilangi amemshukuru Makamu wa Rais kwa maelekezo na kuahidi kwenda kufanya kazi kwa bidii, weledi na maarifa katika kuiwakilisha Tanzania katika nchi hizo.

Mwisho

Post a Comment

أحدث أقدم