Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Augustine Wanyonyi mwenye umri wa miaka 35 amekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuiba Biblia mbili kwenye duka kubwa jijini Nairobi Nchini Kenya.
Wanyonyi alikamatwa Jumapili Januari 30,2022 baada ya kupatikana na nakala mbili za biblia zenye thamani ya Shilingi 2,100 za Kenya (48,000Tsh) na kufikishwa Mahakamani Jumannne Februari Mosi 2022.
Kulingana na ripoti ya polisi iliyosomwa na wakili wa Serikali Alice Mathangani mbele ya Hakimu Mkuu wa mahakama ya Milimani katika Jiji la Nairobi Susan Shitubi, mshtakiwa alikwenda kwenye duka hilo majira wa saa tisa mchana na kuiba biblia mbili na kuzificha ndani ya suruali yake.
"Alinaswa na kanda ya CCTV ya duka kuu na baadaye kukamatwa na wahudumu wa CCTV baada ya kushindwa kulipia bidhaa sawa na hiyo alipofika kwa kaunta," mwendesha mashtaka alisema.
Mwendesha mashtaka pia aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alikuwa na rekodi ya awali ya wizi wa dukani ambapo alishtakiwa Desemba 2021 lakini akaachiliwa na mahakama nyingine baada ya kuomba msamaha.
Kwa upande wake Wanyonyi ambaye ni mshitakiwa alikiri kosa na kuiambia Mahakama kuwa aliiba Biblia hizo ili asome na kumjua Mungu zaidi.
"Niliiba biblia ili nisome, nielewe na kuhubiri neno la Mungu badala ya kujiua kutokana na matatizo yanayonikabili," Wanyonyi aliambia mahakama.
Alipoulizwa kwa nini aliiba nakala mbili badala ya moja Wanyonyi alijibu kuwa Biblia ya pili alikusudia kwa ajili ya mkewe.
Hakimu Mkuu wa mahakama ya Milimani katika Jiji la Nairobi Susan Shitubi aliamuru ripoti ya kabla ya hukumu iwasilishwe mahakamani ndani ya siku saba ambapo Mshtakiwa Atafikishwa mahakamani na kutolewa hukumu mnamo Februari 16,2022.
Mwisho
إرسال تعليق