Na Steven Nyamiti-WM
Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko amesema Kampuni ya Kabanga Nickel ambayo ni mbia wa Serikali kupitia Kampuni ya Tembo Nickel itatoa fursa zaidi za ajira kwa Watanzania hususan wakazi wa wilaya ya Ngara na mkoa wa Kagera ili washiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji ndani ya kampuni.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Jumatatu Februari 14, 2022 katika kikao na wawekezaji kutoka Kabanga Nickel wanaochimba madini ya Nickel kilichofanyika jijini Dodoma.
Amewataka Watanzania wenye sifa na uzoefu katika fani mbalimbali kujitokeza kuomba nafasi zinazotangazwa na Kampuni ya Kabanga Nickel ili wapate fursa zaidi na kukuza maendeleo.
Aidha, Dkt. Biteko amesisitiza kufuata Sheria za Madini hususan ushirikishwaji wa wazawa kwenye masuala ya manunuzi, ajira na uhawilishaji wa ujuzi (local content).
Pia, Dkt.Biteko amesisitiza Kampuni ya Kabanga kuhakikisha kwamba uchimbaji wa madini unazingatia masuala ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii inayozunguka mgodi (CSR).
Amesema Serikali imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji katika Sekta ya Madini ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji madini kuwa zenye tija kwa nchi na wawekezaji wenyewe kwa kuondoa vikwazo mbalimbali.
Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Tembo Nickel, Benedict Busunzu amesema ajira nyingi zimeanza kutolewa ili watanzania wenye sifa waweze kupata nafasi na kuongeza kuwa fursa zipo wazi na matangazo ya nafasi mbalimbali zimeanza kutangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari.
Wengine, waliohudhulia kikao hicho ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dkt.Mussa Budeba Kamishna wa Tume ya Madini, Prof.Abdulkarim Mruma, na Wataalamu mbalimbali kutoka Wizara na Tume ya Madini.
Kwa upande mwingine, Dkt. Biteko amekutana na Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania (TASPA) kujadili mambo mbalimbali yanayohusu uzalishaji huo.
إرسال تعليق