RAIS SAMIA AMUAGIZA WAZIRI MKUU KUUNDA KAMATI KUCHUNGUZA MAUAJI YALIYOFANYWA NA POLISI



Na Samir Salum

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuunda kamati huru itakayofanya uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi.

Rais Samia ameyasema hayo leo Ijumaa Februari 04, 2022 wakati akiwa Wilayani Magu Mkoani Mwanza akielekea katika sherehe za maadhimisho ya miaka 45 ya CCM mkoani Mara zitakazofanyika kesho Jumamosi Februari 05,2022.



Akizungumzia kuhusu Mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara Rais Samia Amelikosoa Jeshi hilo kwa kuunda kamati ya kutaka kujichunguza.

"Kuna mauaji yametokea Mtwara na kwa taarifa zilizopo ni Polisi ndio lililofanya mauaji. Taarifa niliyonayo ni kwamba Polisi wameunda kamati ya kufanya uchunguzi halafu walete taarifa, Haiwezekani Jeshi lifanye mauaji halafu jeshi lichunguze lenyewe” amesema Rais Samia 

Amesema kuwa amemuelekeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuunda kamati nyingine ambayo itafanya uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi hilo.

Wakati huohuo amelitaka Jeshi la polisi kujitafakari kutokana na mauaji hayo.

"kwa hiyo tutasubiri taarifa ya kamati huru itakayoundwa na Waziri Mkuu ituletee taarifa tulinganishe na ile ya Jeshi la Polisi tuonee taarifa mbili zinasemaje tuchukue hatua muafaka." Amesema Rais Samia

Hivi karibuni askari saba wa Jeshi la Polisi walipandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji ya mfanyaniashara wa madini mkoani Mtwara huku wa nane aliyekabiliwa na tuhuma hizo akijinyonga alipokuwa mahabusu.

Mwisho

Post a Comment

أحدث أقدم