Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel mara baada ya kuwasili katika Makao Makuu ya Baraza hilo Brussels nchini Ubelgiji leo tarehe 15 Februari, 2022.
********
Na Samir Salum
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake
ina mipango ya kuanzisha kiwanda cha kuzalisha chanjo ya magonjwa mbalimbali ikiwemo COVID-19.
Kupitia taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zuhura Yunus imesema kuwa Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Februari 15, 2022 katika mazungumzo yake na Rais wa Baraza la umoja wa Ulaya (European Council), Charles Michel wakati wa ziara yake Nchini Ubelgiji.
Rais Samia amesema sababu ya kutaka kujenga kiwanda cha chanjo ni kutokana na gharama za kununua chanjo zilizowekwa na bajeti ya Serikali ya Tanzania zinakadiriwa kuongezeka kutoka shilingi bilioni 26.1 kwa Mwaka 2020 hadi kufikia shilingi bilioni 216 ifikapo Mwaka 2030.
"Tanzania inaomba kuwasilisha mapendekezo,natarajia mtawezesha jambo hili kuwa mradi wenye manufaa, naamini mpango huu utakapotekelezwa utafungua fursa mpya za kuimarisha mahusiano yetu" Amesema Rais Samia
Aidha Rais Samia ameusihi Umoja wa Nchi za Ulaya kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Nchi ya Burundi katika kuimarisha mazingira na kuleta utilivu ndani na nje ya Nchi hiyo kwani umoja huo una ushawishi mkubwa hata kwa jumuiya nyingine.
"Burundi tulivu ina manufaa kwa Maziwa Makuu, nzuri kwa Umoja wa Ulaya na Duniani kwa ujumla"Amesisitiza
Tangu kuanzishwa Rasmi kwa Ushirikiano mwaka 1975 Tanzania imepokea Zaidi ya Euro Bilioni 2 sawa na shilingi trilioni 5 huku Umoja wa Ulaya ukiendelea kuwa washirika wa Kimkakati na maendeleo kwa Tanzania.
Mwisho
إرسال تعليق