TVLA KUONGEZA WIGO WA KUFANYA VIPIMO UBORA WA VYAKULA VYA MIFUGO

Kutoka kushoto ni Mkaguzi wa Vyakula vya Mifugo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Bi. Theodora Baziwe, akifuatiwa na Fundi Sanifu Maabara kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Bw. Henry Mlundachuma, wakizungumza na mfugaji Bw. Erasto Mbise, walipomtembelea nyumbani kwake katika Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam leo Jumatatu Februari 14, 2022 ili kujiona shughuli za ufugaji na vyakula vya mifugo anavyotumia ikiwa ni sehemu ya kuhakiki ubora wa vyakula vya mifugo zoezi lililofanywa katika wilaya za Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA. 
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi, akizungumza ofisi kwake jijini Dar es Salaam, juu ya mipango ya TVLA katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 kuongeza wigo wa kufanya vipimo vya ubora wa vyakula vya mifugo ili kubaini aina za sumu kuvu ambazo zinaweza kusababisha madhara ya usugu wa dawa kwa binadamu na mifugo.
Afisa Mifugo Mtafiti Mkuu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Bi. Wende Maulaga leo Jumatatu Februari 14, 2022 akizungumza na mzalishaji wa vyakula vya mifugo katika Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam wakati wa zoezi la uhakiki ubora wa vyakula vya mifugo katika wilaya hiyo. Zoezi hilo limefanywa katika wilaya za Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA.

Kutoka kulia ni Bw. Martin Ngh’oni ambaye ni mfugaji katika Wilaya ya Ubungo Mkoani Dar es Salaam, akizungumza na Dkt. Evaline Mfuru na Dkt. Scholastica Doto kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) na Bw. David Mbena Mkaguzi wa Vyakula vya Mifugo Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, juu ya upatikanaji wa vyakula vya mifugo pamoja na malighafi zinazotumika kuzalisha vyakula hivyo, wakati wa zoezi lililofanywa na wataalamu kutoka TVLA kukagua ubora wa vyakula vya mifugo na kuwatembelea wafugaji katika wilaya za Temeke na Ubungo. 

*******

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imesema katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 inatarajia kuongeza wigo wa kufanya vipimo vya ubora wa vyakula vya mifugo ili kubaini aina za sumu kuvu ambazo zinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu na mifugo.

Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi amebainisha hayo  ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati wa zoezi la kuhakiki ubora wa vyakula vya mifugo vinavyozalishwa hapa nchini lililofanyika mwishoni mwa wiki, zoezi ambalo limefanywa katika wilaya za Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA.

Dkt. Bitanyi amesema wakala hiyo inatarajia pia kupima mabaki ya ‘antibiotic’ na dawa nyingine za mifugo ndani ya vyakula vya mifugo ili kuhakikisha ubora wa vyakula vya mifugo kwa kutokuwa na mabaki ya dawa ambazo zinaweza kusababisha usugu wa dawa kwa mifugo pamoja na binadamu atakayetumia mazao yanayotokana na mifugo hiyo.

Katika hatua nyingine mtendaji mkuu huyo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), ametoa wito kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo nchini pamoja na wafugaji kuhakikisha wanafikisha sampuli za vyakula katika maabara hiyo ili kupima ubora wa chakula ambacho kinastahili kutumiwa na mifugo pamoja na malighafi ambazo zitatumiwa katika kutengeneza vyakula hivyo.

Amebainisha kuwa matumizi ya vyakula sahihi vya mifugo ambavyo vina virutubisho vinavyostahili, vitamuwezesha mfugaji kufuga kwa tija kwa kuwa mifugo itakuwa katika muda unaotakiwa kitaalamu na kufikia kiwango cha uzito unaotakiwa sokoni.

Akizungumza wakati wa zoezi la kukagua ubora wa vyakula vya mifugo katika Wilaya za Temeke na Ubungo, Afisa Mtafiti wa Mifugo kutoka TVLA Dkt. Evaline Mfuru amesema uwiano sawa wa virutubisho vinavyotakiwa kwenye vyakula vya mifugo kwa kiasi kikubwa hupunguza gharama za uzalishaji pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo.

Nao baadhi ya wafugaji na wazalishaji wa vyakula vya mifugo wamesema zoezi la uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo litakuwa na tija kwa kuhakikisha vinapatikana vyakula bora, ambavyo vitaleta tija kwa mfugaji pamoja na kuondoa sokoni vyakula vya mifugo ambavyo havikidhi vigezo.

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo iko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya uchunguzi wa ubora wa vyakula vya mifugo ili vyakula hivyo viwe katika viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya matumizi ya mifugo na kuleta tija kwa mfugaji.

Mwisho

Post a Comment

أحدث أقدم