Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na msako uliofanywa na Polisi kwa lengo la kudhibiti uhalifu, likiwemo tukio la kuuawa mtoto wa miaka 14 wilayani Sikonge Januari 21.
Katika tukio hilo, msichana huyo anadaiwa kuuawa na kisha baadhi ya viungo vyake zikiwemo sehemu za siri kuondolewa na wauaji wake.
"Mara baada ya tukio hilo ufuatiliaji ulianza mara moja na kufanikiwa kuwakamata watu watatu waliotiliwa shaka. Katika mahojiano dhidi yao walimtaja mganga waliyedai kuwa anahusika na kununua viungo vya binadamu.
“Jitihada zilifanyika na hatimaye alikamatwa na baada ya kufanyiwa mahojiano alikiri kuwa huwa anapelekewa viungo vya binadamu ambavyo ni sehemu za siri za mwanamke, sehemu za siri za mwanaume na kumtaja mtu anayempelekea," amesema Kamanda Abwao.
Mtuhumiwa huyo aliyekuwa anampelekea mganga huyo damu na viungo vya binadamu naye amekamatwa na katika mahojiano ya awali amekiri kuhusika katika utendaji wa matukio ya mauaji maeneo mbalimbali.
Kamanda Abwao ameeleza kuwa, mtuhumiwa ameeleza kuwa huwa anapata damu kutoka kwa watu kwa kuwachoma na kitu chenye ncha kali katika shingo na kukinga damu inayoruka katika chupa ndogo na kisha damu hiyo huuzwa kiasi cha Sh600,000 kwa chupa.
Ameongeza kuwa mbali ya damu pia huchukua baadhi ya viungo vya miili yao hasa sehemu za siri ambavyo wanavipeleka kwa waganga wa kienyeji ambao ndio wanaowaagiza na kisha kuwalipa fedha kulingana na makubaliano.
Ameeleza kuwa, katika mahojiano hayo mtuhumiwa huyo amewataja watu wengine ambao anashirikiana nao katika utekelezaji wa mauaji hayo na upelelezi unaendelea ili kufikia lengo la kuukamata mtandao wote wa watu wanaohusika na mauaji hayo.
إرسال تعليق