WAZIRI MASAUNI ATOA MAAGIZO HAYA KWA IGP SIRRO DHIDI YA POLISI WASIO NA MAADILI


 Na WMNN, Kilimanjaro

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, kumletea majina ya askari Polisi wanaojihusisha na matukio yasiyo ya maadili ili aweze kuwashughulikia.

Amesema lengo la kuwashughulikia askari hao wasiowaadilifu ambao ni wachache ndani ya Jeshi hilo kutasaidia kuwa na Jeshi imara, safi na kulifanya liwe hilo na jamii.


Akizungumza hayo leo Jumamosi Februari 12, 2022 wakati akifunga Mafunzo ya Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi katika Kambi ya Polisi ya Kilelepori, Wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro Masauni amesema yeye ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ambayo inashughulikia nidhamu ya Askari, hivyo atawashughulikia askari hao ambao hawana nidhamu.

“Katika kipindi hiki mimi ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi kama kuna askari ambaye atakuwa anafanya vitu vya hovyo, IGP mlete tu tumalizane naye, hatuwezi kucheka na vitu ambavyo havina maslahi na tija katika nchi hii, tutaendelea kusimamia kwelikweli nidhamu, ni kwa dhamira njema kwa wengi ninyi mliowasafi,” alisema Masauni.

Masauni aliongeza kuwa nidhamu ya Askari ni muhimu katika Jeshi la Polisi kwasababu wanategemewa katika jamii na pia wananchi wana imani kubwa na askari, hivyo inasikitisha sana kuona askari anaenda kuua raia, askari anatoa siri jambo hilo amesema halikubaliki ndani ya Jeshi hilo.

“Inasikitisha leo kunakuwa na askari anaenda kuua raia, hata kama ni mmoja, inasikitisha kuna askari leo anapora, askari anabambikia kesi mtu, aibu na dhambi kubwa, askari anatoa siri kwa wahalifu, lazima tufuate maadili, hili halikubaliki na tutawashughulikia wanaofanya matukio hayo, lazima tusimamie nidhamu ya Jeshi,” alisema Masauni.

Kwa upande mwingine Masauni amesema matukio ya mauaji yanayoendelea nchini pamoja na baadhi ya Polisi wanaojihusisha na matukio ya uhalifu yanamfanya hakose usingizi hivyo amewataka askari kuwa waadilifu.

Ameongeza kuwa tangu ateuliwe kuiongoza Wizara hiyo ambapo sasa amefikisha mwezi mmoja lakini masuala ya mauaji pamoja na baadhi ya polisi hao kushiriki katika masuala ya uhalifu yanamkosesha usingizi na pia hata Rais Samia Suluhu Hassan naye anakosa suingizi kutokana na matukio hayo.

“Mimi tangu nimeingia ndani ya Wizara hii kwa kipindi hiki cha muda mfupi kama mwezi mmoja hivi, kuna vitu wiwili vikubwa vinanikosesha sana usingizi, na si mimi tu nina uhakika Amiri Jeshi Mkuu Rais Samia Suluhu Hassan, naye anakosaa usingizi, na pia na Watanzania wote waliowema, wazalendo, wanaoipenda nchi yao, watakua wanakosa usingizi. Matukio hayo la kwanza ni mauaji, mara utasikia kachinjwa mtu, ukiuliza sababu unaambiwa sababu ya mapenzi, mara kaenda kwa mganga kadhulumiwa, pamoja na sababu nyingi tu,” alisema Masauni.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro amesema zipo changamoto kama uhalifu unaovuka mipaka, ugaidi na na makosa ya dawa za kulevya kwakushirikiana na vyombo vingine ya ulinzi na usalama vimeendelea kudhibitiwa licha ya kwamba bado zipo changamoto nyingine ikiwemo mmomonyoko wa maadili kwenye jamii.

“Mheshimiwa Waziri tunaendelea kupambana na uhalifu unaovuka mipaka, ugaidi na na makosa ya dawa za kulevya kwakushirikiana na vyombo vingine ya ulinzi na usalama, pia bado zipo changamoto nyingine ikiwemo mmomonyoko wa maadili kwenye jamii,” alisema IGP Sirro.


Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro SACP, Ramadhani Mungi amesema jumla ya wanafunzi 1955 wamehitimu mafunzo ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi na kwamba wahitimu hao wamejifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na makosa ya uhalifu na wahalifu.

MWISHO

Post a Comment

أحدث أقدم