DKT. MABULA KUANZA UKAGUZI WA MAENEO YA UWEKEZAJI NCHINI




Na  WANMM DODOMA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema wizara yake itaanza ukaguzi na kuyatambua maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji nchini.

Dkt Mabula amesema hayo leo Jumatano Februari 09,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.


Amesema kuwa wizara yake inatakiwa kukagua na kuyatambua maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na yafanyiwe ukaguzi na kuyatambua ili kupunguza muda kwa mwekezaji kusubiri.

‘’Maeneo haya lazima tuyafanyie ukaguzi pamoja na kuyatambua hasa yale ya vijijini ambayo ardhi yake inahitaji uzalishaji ili kupunguza muda wa mwekezaji kusubiri pale anapohitahitaji ardhi ya kufanya uwekezaji’’  Dkt Mabula

Amesema kuwa Vipaumbele vya Wizara haviwezi kwenda tofauti na vipaumbele vya Rais ambaye ameelekeza suala zima la uwekezaji.

"Sisi kama Wizara tutafanya ukaguzi wa maeneo yote yaliyotengwa tuyatambue na tujue wenzetu wa TIC, TAMISEMI, EPZA ardhi walionayo ni kiasi gani na wamepanga kufanya nini’’ alisema Dkt Mabula

Dkt Mabula ambaye amechukua kijiti cha uwaziri kutoka kwa William Lukuvi alisema, jukumu la Wizara ya ardhi litakuwa ni kutwaa maeneo hayo ili yawe chini yha serikali ili muwekezaji atakapofika serikali itajua sehemu sahihi kumpeleka kwa kuwa kutakuwa na kanzidata ya maeneo husika.

‘‘Kwenye maeneo ya Vijiji kuna maeneo mengi ambayo yana fursa nzuri za uwekezaji ambapo ardhi ya vijiji inasimamiwa na Sheria Na. 5 ili iweze kumilikiwa inabidi zoezi la uhaulishaji katika maeneo yaliyokusudiwa kuwa ya uwekezaji lifanyike kwa ukamilifu na kuwe na umiliki wa eneo ili mwekezaji atakapokuja tusianze kufanya mikutano ya wananchi ili wakubali’’ alisema Dkt Mabula .

Akigeukia suala la migogoro ya Ardhi, Dkt Mabula alieleza kuwa migogoro ya ardhi inagusa Wizara tano za Kisekta na inatokea kwa sababu hapajaweza kuwekewa mpango wa matumizi ya ardhi kwa nchi nzima na kubainisha kuwa, wizara itazungumza na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa maana ya halmashauri zote ili kuweza kuona kwa jinsi gani patakuwa na zoezi la maksudi kabisa la kuhakikisha kwamba walau vijiji na maeneo mengi yanapangiwa matumizi ya ardhi.

‘‘Bila kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi migogoro haiwezi kuisha na tukipanga na kuheshishimu makubaliano yaliyowekwa katika maeneo hayo ni wazi migogoro itapungua, ili kufanikisha hili inahitaji ushirikiano wa Wizara Tano za Kisekta’’ alisema Dkt Mabula.

Kwa upande wa zoezi la anuani za makazi, Waziri wa Ardhi alisema kipaumbele cha Wizara yake itakuwa kwenda kwa kasi kubwa katika suala zima la upimaji maeneo pamoja na kutambua wamiliki wa maeneo hayo. ‘’Kwetu sisi Wizara katika zoezi la anwani za makazi limepewa kipaumbele kikubwa kwamba tukizembea tutakuwa tumekwamisha zoezi zima’’ alisema Dkt Mabula.

Mwisho

Post a Comment

أحدث أقدم