Kwa mujibu wa vyombo vya habari shambulio hilo limetokea leo Alhamisi Februari 10,2022 wakati waziri mkuu huyo wa mpito alipokuwa anarudi nyumbani kwake.
Imeelezwa kuwa risasi moja ilipenya kwenye kioo cha gari iliyombeba Dbeibah, lakini yeye na dereva wake hawakudhurika huku ikielezwa kuwa risasi zilikuwa za silaha nyepesi, na uwezekano mkubwa ni aina ya Kalashnikov.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini libya vimesema kuwa Mwendesha mashtaka mkuu wa Libya ameanzisha uchunguzi kuhusu shambulio hilo japo Ofisi ya waziri mkuu bado haijatoa taarifa.
Jaribio hilo la mauaji limetokea huku kukiwepo na misuguano na mivutano mikali ya kimirengo juu ya udhbiti wa serikali ya mpito ya Libya, ambapo waziri mkuu huyo aliyechaguliwa mwaka uliopita ameahidi kuwa atapambana na hatua za wapinzani wake wenye lengo la kumng'oa katika wadhifa huo.Dbeibah, ambaye ni mfanyabiashara mkubwa kutoka mji wa Misrata, alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mwezi Machi 2021, na kukabidhiwa jukumu la kuongoza nchi hiyo kuelekea uchaguzi mkuu ambao ulikuwa umepangwa ufanyike Desemba 24 .
Alikabidhiwa wadhifa huo kwa sharti la kutogombea urais, hata hivyo mnamo mwezi Novemba, Abdulhamid Dbeibah, alitangaza nia ya kugombea, hatua ambayo ililalamikiwa na baadhi ya mirengo.
Wabunge wa Libya wamepanga katika kikao chao cha leo kuteua waziri mkuu mpya wa mpito, kati ya aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Fathi Bashaga na aliyekuwa afisa katika wizara hiyo Khaled al-Bibass, uamuzi ambao Dbeibah amesema atakabaliana nao na kusisitiza kwamba, hatakabidhi madaraka isipokuwa kwa serikali itakayochaguliwa tu.
Endapo bunge litachukua hatua hiyo, Libya itaingia tena kwenye kizungumkuti cha mwaka 2014 cha kuongozwa na serikali mbili kwa wakati mmoja.
إرسال تعليق