MKAZI wa Newland Kijiji cha Mvuleni, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Grace Pima, anadaiwa kumchoma moto mtoto wake wa miaka mitano mdomo pamoja na pua.
Mama huyo anadaiwa kutekeleza kitendo hicho kwa kutumia banio linalotumiwa kuunganisha njia ya reli, pia inadaiwa alimfungia ndani mtoto huyo ambaye ni wa kiume (jina limehifadhiwa) kwa takribani saa 48.
Ukatili huo ulifichuliwa jana na Mjumbe wa Kamati ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), Agness Moshi, wakati wa kikao kazi cha Mradi wa Paza Sauti, Tokomeza Ukatili, unaoendeshwa na Shirika la TUSONGE CDO.
Agness alisema mama huyo baada ya kutekeleza ukatili huo, anadaiwa kumficha ndani mtoto huyo na kuanza kumtibu majeraha kwa dawa za kienyeji, akiwa amemsiliba mdomoni na puani, majani mabichi yaliyotafunwa yanayodaiwa kuwa ni dawa.
“Tulipomkamata na kumuuliza kwa nini amemchoma mtoto wake, alituambia kwamba mtoto alitoa tusi. Nikamuuliza ni tusi gani hajielezi kitu kinachoeleweka.
“Huyu mama alifanya ukatili huo Februari 28, usiku na sisi tulipata taarifa kutoka kwa majirani zake Machi 2, mwaka huu, baada ya kumfungia ndani kwa saa 48 akimtibu kwa dawa za kienyeji za mitishamba ili asibainike.
Alisema baada ya kupata taarifa hiyo walimchukua mama na mtoto na kuwapeleka Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Mvuleni
Agness alisema baadaye waliondoka na mtoto kwenda Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Kilimanjaro ya Mawenzi ili akapatiwe matibabu.
Alieleza kwamba mama anayedaiwa kutekeleza kitendo hicho walimpeleka Dawati la Jinsia la Polisi, Wilaya ya Moshi na walipewa fomu namba tatu kwenda Mawenzi.
Alieleza kuwa hivi sasa mama huyo anashikiliwa kituo cha polisi, kwamba anaendelea kuhojiwa.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Moshi, Habiba Bhou, alisema: “Sisi tunatoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi, kwa sababu ukisoma kwenye elimu ya malezi na makuzi, hilo tukio la mama kumchoma mtoto wake mdomo na pua ili asimtukane, iko namna.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mvuleni, Kata ya Mabogini, Veronica Mjinja, alisema mama huyo alikamatwa na wananchi wapatao 15 wenye hasira, ambao baada ya tukio hilo walitaka kumdhuru.
Ofisa wa Polisi Kata ya Mabogini, Mkaguzi Msaidizi, Japhary Kalinga, alisema kila mzazi au mlezi anatakiwa kujua kwamba mtoto yeyote mwenye umri chini ya miaka tisa, hata akifanya jambo baya, sheria haimhusishi na makosa ya jinai.
إرسال تعليق