Kamanda wa jeshi la ardhini nchini Uganda UPDF , luteni jenerali Muhoozi Kainerugaba ametangaza kustaafu katika jeshi hilo baada ya kuhudumu kwa miaka 28.
Hata hivyo ombi lake la kutaka kustaafu linatarajiwa kuidhinishwa chini ya kifungu cha sheria za jeshi la UPDF 2005.
Aliandiaka katika ujumbe wake wa twitter:
''Baada ya kuhudumu kwa miaka 28 katika jeshi letu , jeshi bora zaidi duniani , nafurahia kutangaza kwamba ninastaafu. Mimi na wanajeshi wangu tumefanikiwa pakubwa , ninawapenda na kuwaheshimu maafisa wote waliofanikiwa kila siku '', alisema mtoto huyo wa rais wa Uganda Yoweri Museveni katika mtandao wake wa twiter.
Muhoozi ambaye alipanda ngazi katika jeshi hilo alisema kwamba yeye na wanajeshi wake wamepata mafanikio makubwa.
Kulingana na gazeti la The Monitor nchini Uganda , tayari huduma za mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter na facebook zimetawaliwa na jumbe za Muhoozi kuwa rais mtarajiwa wa Uganda licha ya Muhoozi mwenye umri wa miaka 47 kukataa kutangaza hadharani.
Tayari ujumbe huo umechukuliwa na kuwekwa katika akaunti ya twitter ya jeshi la UPDF.
Kulingana na sheria za jeshi, afisa anaweza kuwasilisha ombi la kustaafu katika bodi lakini hawezi kuondoka jeshini hadi pale ombi lake litakapoidhinishwa na bodi ya jeshi kulingana na kifungu 66{1} .
Nchini Uganda , maafisa wakuu wa jeshi akiwemo jasusi wa zamani wa taifa hilo Jenerali David Sejusa , awali alikataliwa ombi lake la kutaka kustaafu ama hata kucheleweshwa kulingana na gazeti la The Monitor Uganda.
إرسال تعليق