Kampuni ya utangazaji ya satelaiti ya Afrika Kusini Multichoice imetangaza kuacha kutangaza chaneli ya habari inayomilikiwa na serikali ya Russia Today (RT) kwenye jukwaa lake la DSTV hadi itakapotangazwa tena.
Katika taarifa, Multichoice ilitaja vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi ndivyo ambavyo "vimesababisha msambazaji wa kimataifa wa idhaa hiyo kusitisha urushaji wa matangazo hayo kwa wasambazaji wote, ikiwa ni pamoja na Multichoice".
Huduma ya Multichoice ya DSTV inarusha matangazo bara zima.
Inafuatia uamuzi wa Umoja wa Ulaya siku ya Jumatano kusimamisha usambazaji wa matangazo ya kituo cha Russia Today na Sputnik kote katika jumuiya hiyo, ikizitaja njia hizo kama upotoshaji wa habari.
Lakini uamuzi huo wa Multichoice umeshutumiwa na chama cha Wapigania Uhuru wa Kiuchumi yaani Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini, ambacho kilisema huko ni kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na haki za watumiaji.
"Multichoice imechagua ni vyombo vipi vya habari ambavyo watumiaji wanapaswa kutazama na kuamuru ni maudhui gani lazima yatazamwe kulingana na uaminifu wao katika mzozo tata huko Uropa," chama kilisema kwenye taarifa.
Wakati huo huo, ubalozi wa Urusi nchini Uganda ulisema shirika la utangazaji la nchi hiyo, UBC, litarusha matangazo ya Urusi Leo kila siku kwa saa moja asubuhi na usiku sana.
Idhaa ya Russia Today (RT) inajielezea kama yenye kujitegemea inayofadhiliwa na Shirikisho la Urusi.
إرسال تعليق