RAIS ZELENSKY: KUSHINDWA KWA MAZUNGUMZO KUTAMAANISHA VITA YA 3 YA DUNIA..


Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kuwa anaamini kushindwa kufanikisha mazungumzo ya kumaliza uvamizi wa Urusi kutamaanisha "vita vya tatu vya dunia".

Akizungumza na CNN Jumapili, Zelensky alisema yuko tayari kuzungumza moja kwa moja na Rais wa Urusi Vladimir Putin, akiongeza kuwa anaamini kuwa mazungumzo ndiyo njia pekee ya kumaliza mapigano.

"Nadhani tunapaswa kutumia muundo wowote, nafasi yoyote ili kuwa na uwezekano wa kufanya mazungumzo," alisema.

Hata hivyo, Zelensky alisema kuwa anakataa makubaliano yoyote ambayo yangehitaji Ukraine kutambua maeneo yanayojitenga yanayofadhiliwa na Urusi kuwa huru.

Rais wa Ukraine alisema anaamini kwamba kama nchi yake ingekuwa mwanachama wa Nato, "vita havingeanza".

"Ikiwa wanachama wa Nato wako tayari kutuona katika muungano, basi fanya hivyo mara moja," alisema. "Kwa sababu watu wanakufa kila siku".

Hakuna kusalimu amri

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imeutaka mji unaokabiliwa na mgogoro wa Mariupol ujisalimishe ifikapo 05:00 saa za huko Jumatatu asubuhi - pendekezo ambalo Ukraine imekataa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Urusi la Ria Novosti, wizara hiyo imesema kuwa itafungua korido za kibinadamu ili kuruhusu wakaazi kuondoka ifikapo saa 10:00 kwa saa za huko (08:00 GMT) ikiwa itapata jibu la maandishi kwa pendekezo hilo.

Kanali Jenerali Mikhail Mizintsev, mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Usimamizi wa Ulinzi cha Urusi, alinukuliwa na Ria Novosti akisema kuwa maafisa wa eneo hilo watakabiliwa na "mahakama ya kijeshi" ikiwa hawatakubali masharti ya kujisalimisha.

Mapema Jumatatu, Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk alisema kuwa kunaweza kuwa "hakuna swali" la kujisalimisha.

"Tayari tumefahamisha upande wa Urusi kuhusu hili," alinukuliwa akisema na Ukrainska Pravda.

Post a Comment

أحدث أقدم