Polisi wa Kituo Kidogo cha Polisi Uchira, Kata ya Kirua Vunjo Kusini, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wanachangishana kumlipa shilingi 560,000 mkazi wa eneo hilo kabla ya Agosti 5 mwaka huu baada ya kuibwa vitu vyake vilivyokuwa ndani ya kituo hicho.Vitu hivyo vilivyoibwa Julai 26, 2022 ni televisheni, pasi, kisimbuzi cha televisheni pamoja na nyaya za umeme ambavyo vilikamatwa na kuwekwa kituoni hapo kama vielelezo baada ya kuibwa.
"Maaskari wameniahidi kuwa kabla ya ljumaa watanilipa vitu vyangu, na kuwa kwa sasa hawana fedha, kwani mshahara wamemaliza, ila ninachotaka ni vitu vyangu na si kingine, kwa hivyo wanatumia njia mbadala kupata fedha" amesema mmiliki.
Diwani wa kata hiyo, Peter Meela amedai askari aliyekuwa zamu alitoka kidogo kwenda jengo la elimu karibu na kituo hicho cha polisi, ndipo mwizi aliingia kituoni na kuiba vitu hivyo vilivyokuwa vikishikiliwa.
Naye Kamanda wa Polisi mkoani humo, Simon Maigwa amesema huo ni wizi wa kawaida kama wanavyofanya wengine, na tayari mtuhumiwa amekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
Source: Swahili Times
إرسال تعليق