MTENDAJI WA KATA JELA MIAKA 3 KWA KUOMBA RUSHWA.

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilayani Kaliua Mkoani Tabora imemhukumu kifungo cha miaka 3 jela Mtendaji wa Kata ya Nh’wande na mwenzake wa Kijiji cha Imagi baada ya kutiwa hatiani kwa kuomba na kupokea rushwa ya sh. mil 3.

Akitoa hukumu hiyo juzi Hakimu Mkazi Mwandamizi Felix Ginene amesema kuwa ametoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia kama hizo katika Wilaya hiyo na mahali pengine.

Ametaja Mtendaji wa Kata hiyo aliyehukumiwa kuwa ni Laurent Isaya Sendu na mwenzake Richard Mpagama wa Kijiji Cha Imagi kilichoko katika kata hiyo ambao waliomba rushwa ya sh mil 3 kwa mkazi wa Kijiji hicho.

Amebainisha kuwa ni kosa kwa Kiongozi yeyote kutumia madaraka yake vibaya dhidi ya wananchi anawaongoza kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki zao kisheria.

‘Rushwa ni adui wa haki, inapobainika Kiongozi katumia madaraka yake kuomba au kupokea rushwa, sheria itachukua mkondo wake, vitendo vya rushwa havikubaliki mahali popote kwa kuwa vinawanyima haki wananchi’, amesema.

Hakimu Felix amefafanua kuwa awali watuhumiwa walirejesha kiasi cha sh laki 7 kati ya sh mil 3 walizochukua kwa mlalamikiaji Ndilana Budeba wakati wa uchunguzi wa kesi hiyo, hivyo akaagiza kurejeshwa kiasi kilichobaki pia.

Waendesha Mashtaka wa Serikali David Bakari na Kajivo Aidan wameiiambia mahakama hiyo kuwa watuhumiwa walitenda kosa hilo Aprili 21, 2023 ambapo waliomba kiasi hicho cha fedha kwa madai kuwa watamaliza tatizo lake.

Wameongeza kuwa watuhumiwa walimwambia mlalamikaji kuwa akitoa kiasi hicho hawatamfuatilia tena kutokana na kosa alilounganishwa nalo linamhusu mkwe wake (mume wa binti yake) la kuhusika na wizi wa kutumia silaha.

Aidha wameiambia mahakama kuwa kosa hilo la jinai na.71/2023 dhidi ya watuhumiwa Laurent Sendu na Richard Mpagama ni kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha makosa ya rushwa (sura ya 329 marejeo ya mwaka 2022).

Watuhumiwa wote 2 wamehukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya sh mil 1 kila mmoja lakini baada ya kushindwa kulipa faini hiyo wamepelekwa gerezani kutumikia kifungo hicho.

Post a Comment

أحدث أقدم