HALMASHAURI ZIONGEZE KASI UKUSANYAJI MAPATO - RC MTANDA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amezitaka Halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha wanafanya kazi ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuzisaidia Halmashauri zao ziweze kujiendesha na kuepukana na hali ya ukata.

Mhe. Mtanda ametoa wito huo wakati akiongea na watumishi kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Misungwi leo tarehe 07 juni, 2024.

Sambamba na ukusanyaji mapato Mhe. Mtanda pia amewataka Watumishi wa Umma kuzipenda kazi zao kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakizingatia utoaji wa haki kwa wananchi wanaostahili.

"Kazi ndio msingi wa utu, tuzipende kazi zetu, wapo wanaochezea kazi zao kwa kuamua hata kulewa pombe lakini mimi naamini kwenye kazi kupata kipato na kujenga heshima." Mhe. Mtanda.

Aidha, amewataka watumishi wote kusimamia miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati na daima wawe wakweli kwenye utendaji wao  kwani hali hiyo itasaidia kuleta mshikamano utaoimarisha maelewano kazini.

"Mtumishi yeyote wa umma anayetoa huduma bora kwanza atapendwa na viongozi wake lakini pia atapendwa na wananchi, pokeeni wateja kwa utayari kwa kuwasikiliza." Amesema Mkuu wa Mkoa wakati akisisitiza suala la utoaji huduma bora.

Vilevile, amewataka watumishi kwenye idara zao kuhakikisha wanakua na mipango ya muda mfupi na mrefu na kuhakikisha wanaifuata na kuikamilisha ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

"Kufuata maadili ndio msingi mzuri wa kazi, tuwahi kazini na kuhakikisha tutekeleza majukumu yetu tena kwa wakati na sio kuwahi kazini na kushinda tunachezea simu hapana hiyo haikubaliki na tutachelewesha maendeleo kwa wananchi." Mkuu wa Mkoa.

Halikadhalika, ameipongeza halmashauri hiyo kwa kutekeleza vema maagizo ya viongozi kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato hadi kukaribia kukusanya shilingi bilioni 4 tofauti na siku za nyuma ambapo walikua wanakusanya shilingi bilioni 2 pekee.



Post a Comment

أحدث أقدم