Wanafunzi wa shule za sekondari za manispaa ya Ilemela wametakiwa kuzingatia elimu ya darasani na michezo kwa pamoja badala ya kuipa kipaumbele michezo peke yake.
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu Ummy Mohamed Wayayu wakati wa kufunga mashindano ya umoja wa michezo ya shule ya sekondari UMISETA ngazi ya wilaya yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Bwiru wavulana ambapo amewataka wanafunzi kuhakikisha ubora wao katika michezo unaenda sambamba na ubora kitaaluma
'.. Tuzingatie na masomo yetu, ukiwa mwanamichezo mzuri alaf una elimu inapendeza zaidi hata ukichukuliwa huko mbele hauwezi kutetereka ..' Alisema
Aidha Ndugu Wayayu ameitaka timu ya manispaa ya Ilemela kuhakikisha inarudi na ushindi kwa kubeba vikombe vyote vya mashindano ya michezo kwa ngazi ya mkoa ikiwa pamoja na kuwa na nidhamu wakati wote wa mashindano
Kwa upande wake afisa michezo wa manispaa ya Ilemela Mwalimu Kizito Bahati Sosho akasema kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa kuunda timu ya wilaya watakuwa kambini kwa siku tatu kabla ya kuanza mashindano ya ngazi ya mkoa na kwamba kipindi chote watakachokuwa kambini sheria na taratibu za shule zitaendelea kufuatwa na mwanafunzi yeyote atakaekiuka atachukuliwa hatua za Windhamu.
Mwalimu Jane Joseph kutoka shule ya sekondari Sangabuye ndie aliechaguliwa kuwa mlezi wa timu hiyo ya wilaya yenye jumla ya vijana zaidi ya 120 ambapo amewahakikishia wazazi kusimamia maadili, afya, usalama na malezi ya wanafunzi kwa kipindi chote watakachokuwa katika mashindano
Sada Yusuph ni kati ya wanafunzi waliochaguliwa kuunda timu ya wilaya kuwakilisha mkoa ambapo ameahidi kujituma na kufanya vizuri katika mashindano hayo huku akiwaasa wale wanafunzi waliokosa nafasi kuunda timu hiyo kutohisi hawana uwezo badala yake kujipanga kwa awamu nyengine kwani nafasi ni chache na wanafunzi wenye vipaji ni wengi
Mpaka kutamatika Kwa mashindano hayo ngazi ya wilaya, Timu ya kanda ya Bugogwa iliweza kufanikiwa na kuwa mshindi wa jumla huku mashindano ya UMISETA kwa mwaka 2024 yakipambwa na kauli mbiu ya " Tunajivunia mafanikio katika sekta ya elimu, michezo na sanaa hima mtanzania shiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 "
إرسال تعليق