Kufuatia ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda aliyoifanya Mei 24, 2024 kukagua huduma mbalimbali zinazotolewa na Hospitali ya Kanda ya Jeshi la Wananchi Mwanza iliyopo wilayani Ilemela, wananchi kutoka maeneo mbalimbali wameanza kufika ili kupata matibabu ya kibingwa huku wakipongeza viwango vya utoaji wa huduma hizo.
Hayo yamedhihirika baada ya Bi. Dina Mgeta kutoka Mkoani Mara kufika kwenye hospitali hiyo mnamo Mei 31, 2024 akiwa na uvimbe usio wa kawaida shingoni ili kupata matibabu ambapo leo Juni 04, 2024 mgonjwa huyo amezungumzia furaha yake baada ya kufanyiwa upasuaji wenye mafanikio na hali yake kuwa nzuri.
Mgonjwa huyo amemshukuru Mkuu wa Hospitali hiyo kwa ukarimu na moyo wa kiungwana kwani mara tu baada ya kumpokea alihakikisha anamhudumia hata baada ya kubaini kuwa mgonjwa huyo aliyeletwa na mama yake mzazi kutokua na fedha za matibabu wala bima ya afya hivyo kulazimika kuomba kupatiwa matibabu kwa msamaha.
Mgonjwa huyo ameonesha furaha yake kutokana na kupata matibabu mazuri ya kibingwa na akatumia wasaa huo kutoa wito kwa wananchi wengine kuhakikisha wanakata Bima ya Afya kwani inasaidia sana endapo unapata maradhi na kuhitaji matibabu jambo ambalo yeye alishindwa kufanikisha kutokana kutokuwa na bima ya afya.
Mkuu wa Hospitali ya Kanda ya Jeshi Mwanza ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji na ndiye aliyemfanyia Upasuaji mgonjwa huyo, Luteni Kanali Ahmed Shabhay amesema walimpokea mama huyo akiwa na uvimbe mkubwa shingoni (Huge Multi-nodular Goiter) na alihitajika kufanyiwa upasuaji wa kutoa uvimbe huo.
Amesema, Mama huyo hakuwa na fedha za matibabu na wala hakua mnufaika wa bima ya afya na aliifikisha changamoto yake kwenye uongozi wa hospitali nao kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa walifanikisha na kumfanyia upasuaji Mei 31,2024 ambao umeenda salama kutokana na vifaa tiba na wataalamu tiba na kwamba kwa sasa yupo salama na ameruhusiwa kwenda nyumbani kwani matibabu hayo yamekamilika.
Luteni Kanali Ahmed Shabhay ametoa wito kwa wananchi kutoka Mwanza na mikoa ya jirani kufika kwenye hospitali hiyo kupata matibabu ya kibingwa kwani wana watoa huduma wabobevu na vifaa vya Kisasa na kwamba wanahudumia Maafisa, Askari na familia zao pamoja na raia kwa njia zote za malipo ya papo kwa papo na Bima ya afya.
إرسال تعليق